RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameupa wiki moja uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, kuwapatia viwanja vya kujenga nyumba wahanga wa mafuriko ya kiasi cha miaka minne iliyopita mjini Kilosa.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo, Agosti 24, 2014 wakati alipozungumza na wananchi wa Kilosa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kilosa baada ya kutembelea Wilaya hiyo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete amerejea Mkoani Morogoro asubuhi ya leo kuendelea na ziara yake ya siku saba mkoani huo baada ya kuikatisha jana, Jumamosi, Agosti 23, 2014, kwenda kwenye Chuo cha Uongozi wa Kijeshi, Monduli, Mkoani Arusha, ambako alikwenda kutoa kamisheni kwa maofisa wapya wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF).
Baada ya kuwa amelalamikiwa kwa maneno na kwa mabango na wahanga hao kuwa hawajapatiwa viwanja vya kujenga nyumba za kudumu baada ya kuwa wameahidiwa viwanja hivyo na Rais Kikwete mwenyewe wakati alipowatembelea kufuatia mafuriko ya Mto Mkondoa miaka minne iliyopita, Rais Kikwete amesema:
“Ni jambo la kusikitisha kuwa bado ahadi zangu kwenu hazijatimizwa. Niliahidi mambo mawili wakati nilipokuja kuwaoneni – moja niliahidi kuwa tutawapatia viwanja vya kuweza kujenga nyumba za kudumu na pili niliwaahidi kuwasaidia kujenga nyumba. Sasa tuanze na la kwanza,”alisema Rais Halmashauri hiyo kujieleza mbele ya wananchi hao kuhusu ahadi hizo.
Baada ya kuambiwa kuwa vimepimwa viwanja 800 katika Halmashauri hiyo, Rais Kikwete aliamuru kuwa kiasi cha viwanja 400 vitengwe kwa ajili ya wahanga hao wa mafuriko.
“Katika muda wa wiki moja, yaani kuanzia kesho Jumatatu hadi kufikia Ijumaa, nataka taratibu zote kuwa zimekamilika na kila mtu kuwa ameonyeshwa kiwanja chake. Tutazingumzia habari ya ujenzi baadaye,” alisema Rais Kikwete.
Mapema asubuhi, Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme katika eneo la Msolwa, Wilaya ya Kilosa, mradi ambao unajengwa na Shirika la Watawa wa Madonda Matakatifu ya Yesu la Stigmatine Fathers and Brothers la Kanisa Katoliki ambalo lilianza shughuli zake katika Wilaya ya Kilosa Novemba 1989.
Mradi huo wa Yovi Mini Hydropower Project unajengwa kwenye milima na maporomoko ya Mto Yovi na unalenga kuzalisha megawati kati ya moja na 2.3 kwa ajili ya mamia kwa mamia ya watumiaji katika eneo hilo ikiwamo shule maarufu na ya mfano ya sekondari ya Msolwa St. Gaspar iliyofunguliwa na Shirika la Stigmatine mwaka 1994.
Mradi huo ambao unagharimu Sh. bilioni tisa utaondoa gharama kubwa za kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli, utawezesha Shule ya Msolwa kuwa na umeme wa uhakika, utawezesha wananchi za vijiji vya Kisanga, Msolwa na Madizini kupata umeme wa uhakika kwa bei nafuu na utaunganishwa moja kwa moja kwenye gridi ya taifa katika jitihada za kupunguza tatizo la umeme nchini.
Gharama za umeme huo ambao utaanza kuzalishwa Januari mwakani zimechangiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mradi wa Umeme Vijiji – REA- na wananchi wa eneo hilo ambao wametoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi. Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Morogoro leo.