*Akutwa na silaha ya kivita
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
ASKARI wa Jeshi la Polisi mkoani Dodoma ambaye ni mtunza silaha wa Wilaya ya Dodoma mjini, Meja George Andala pamoja na raia sita wamekamatwa katika pori la Hifadhi ya Taifa lililopo wilaya ya Chamwino wakiwinda wanyama bila kibali kwa kutumia sila ya kivita.
Taarifa za uhakika ambazo mtandao huu umezipata, Meja Andala ambaye alikamatwa na silaya kubwa ya Jeshi la Polisi, aina ya G3 alikamatwa na kikosi maalumu cha kuzuia uhalifu nchini akiwa katika pori hilo. Taarifa zaidi zinasema Meja Andala ambaye pia kimajukumu ni Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Wilaya ya Dodoma na amekamatwa akifanya kosa hilo akiwa katika likizo ya kustaafu aliyoianza tangu Juni, 2014.
“…Tumemkamata akiwa na vijana wengine sita ambao walikuwa pamoja wakifanya uhalifu huo, wote bado tunawashikilia kwa uchunguzi zaidi,” kilisema chanzo chetu cha habari japokuwa kiligoma kutaja eneo ambalo kwa sasa watuhumiwa wanashikiliwa.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu mjini hapa umegunduwa Meja Andala na raia wenzake 6 wako mahabusu ya Jeshi la Polisi Wilaya ya Chamwino na juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi kuzungumzia tukio hilo ziligonga mwamba. Hata hivyo bado mwandishi wetu anaendelea kumtafuta kwa ufafanuzi zaidi.
Matukio ya uwindaji haramu yamekuwa yakiendelea kushamiri katika hifadhi mbalimbali za taifa huku yakiteketeza wanyama na uharibifu mkubwa katika hifadhi hizo. Hata hivyo vitendo vya uwindaji haramu vimekuwa vikihusishwa na viongozi na watendaji wa Serikali ambao wanafadhili mitandao hiyo ya uwindaji. Taarifa zaidi juu ya tukio hilo endelea kufuatilia hapahapa dev.kisakuzi.com.