KOZI YA MAKAMISHNA WA MPIRA WA MIGUU

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

KOZI ya makamishna wapya kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Taifa na Kombe la Taifa itafanyika ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Agosti 6-8 mwaka huu.

Kwa wanaotaka kuwa makamishna ni lazima washiriki katika kozi ambapo ada ni sh. 10,000. Washiriki wanatakiwa kuwa waamuzi wastaafu na viongozi (administrators) wa mpira wa miguu katika ngazi mbalimbali. Pia wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao halisi (original) vya elimu.

Kutakuwa na mitihani ya kuandika ya sheria za mpira wa miguu na picha (video clips) ambapo watakaofaulu watapata vyeti.

Kwa upande wa makamishna waliopo sasa wa Ligi Kuu, wao watahudhuria kozi hiyo kwa siku moja (Agosti 8 mwaka huu). Kozi itaanza saa 2 asubuhi hadi saa 11 jioni. Washiriki wote wanatakiwa kujitegemea kwa usafiri, chakula na malazi kwa muda wote wa kozi hiyo.

Wakufunzi wa kozi hiyo watakuwa Kapteni mstaafu Stanley Lugenge, Joseph Mapunda na Leslie Liunda.