Zao la alizeti linaweza kukuza uchumi wa Tanga

Zao la alizeti likiwa shambani

Na Ngusekela David, Tanga

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Seif Mpembenwe amesema wakulima wa alizeti wataweza kuinua kipato chao mara dufu endapo watalima zao hilo la alizeti kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora.
Mpembenwa alisema hayo mjini hapa alipokuwa akifungua kikao cha pili cha jukwaa la wadau wa alizeti wilayani Handeni, ambalo limeundwa kwa lengo la kuwaunganisha wadau wa zao hilo, mradi unaoratibiwa na Muungano wa Wajasiriamali Vijijini (MUVI).
Mpembenwe amesema Wilaya ya Handeni ina ardhi kubwa yenye rutuba, na kuwataka wakulima waache tabia ya kilimo cha mazoea na badala yake kuongeza ukubwa wa mashamba na kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo, jambo ambalo litawasaidia kuongeza kipato na kujikwamua na umasikini.
Alisema ujio wa MUVI umeleta tija kwa wakulima pamoja na hamasa ya kilimo cha alizeti. Aliongeza kuwa wakulima wakulima eneo hilo wamelima jumla ya hecta 476, ukilinganisha na lengo la hecta 403.2 walilojiwekea awali.
Aidha wilaya hiyo ikishirikiana na mradi wa MUVI imefanikiwa kuwapeleka wasindikaji wa alizeti Mkoa wa Morogoro mapema mwaka huu na kujifunza teknolojia. Mbali na mafunzo hayo ziara imezaa matunda kwani hadi sasa jumla ya mashine tatu za kukamulia mafuta zimefungwa moja ikiwa Kabuku na nyingine mbili Chanika.
Hata hivyo Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na MUVI imefanikiwa kuwaunganisha wakulima wa alizeti kutoka kata za Vibaoni na Amani na taasisi za fedha ambapo wamefanikiwa kupata mikopo pamoja na kuwaunganisha na wanunuzi wa mazao.
Akizungumza Ofisa Mradi wa MUVI, Patrick Mujuni amesema katika kipindi cha mwaka 2011/2012, MUVI imepanga kuwafikia wakulima wote wa alizeti wa kata za Sindeni, Kwamgwe, Segera. Kata zingine ni Kwamatuku, Vibaoni, Chanika Chogo, Kang’ata, Kwalugulu Mazingara, Misima Ndolwe na Kabuku.
MUVI itasimamia na kuimarisha vikundi vya wadau wa alizeti ili kusaidia upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima na kubadilisha mfumo wa kilimo kutoka mkulima mdogo hadi wa kati na kufanya masoko ya ndani kuwa endelevu na yenye tija.
“Vile vile MUVI itawajengea uwezo watendaji wa msingi katika sekta ya alizeti kwa kuandaa na kuwepo kwa vijarida/vitabu elekezi vya kilimo kama biashara na kilimo bora cha alizeti,” amesema Mujuni.
Baadhi ya wakulima wa eneo hilo wakitoa maoni yao walisema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa tofauti na hapo nyuma. Mwanaisha Hussein mmoja wa kulima eneo hilo alisema miaka ya nyuma alikua akilima alizeti nusu eka na mwaka jana alivuna debe mbili, lakini kufuatia uhamasishaji unaofanywa na mradi wa MUVI sasa amelima ekari moja na tayari amevuna na kupata mafanikio zaidi.