MCHAKATO WA MAOMBI YA MIKOPO KWA MWAKA WA MASOMO 2014/2015
1.0 MAANDALIZI YA UTOAJI MKOPO KWA MWAKA WA MASOMO 2014/2015
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilitangaza mwongozo na vigezo vya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 kupitia magazeti na tovuti yake mnamo wezi Aprili 2014. Mwongozo huo, pamoja na mambo mengine, uliainisha sifa za waombaji mikopo na ruzuku, vipengele vya Mikopo, programu za vipaumbele kwa waombaji wa shahada ya kwanza, shahada za uzamili na uzamivu waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu zinazotambulika. Maombi ya mikopo kwa waombaji wapya yalifanyika kwa njia ya mtandao kwa anuani ya http://olas.heslb.go.tz au kupitia anuani ya tovuti ya Bodi ya Mikopo ambayo ni: www.heslb.go.tz.
Kulingana na Mwongozo wa Utoaji Mikopo na Ruzuku kwa mwaka wa masomo 2014/2015, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilifungua maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao (OLAS) kuanzia Aprili 23, 2014 na kuendelea kupokea maombi hayo hadi Julai 31, 2014.
Mabadiliko machache yamefanyika, kubwa likiwa ni kwa wanufaika wanaoendelea na masomo, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita, hawakutakiwa kujaza tena fomu kuthibitisha uhitaji wao wa mikopo kwa mwaka unaofuatia, isipokuwa kwa wale ambao waliopenda kusitisha kuendelea kupokea mkopo kutoka Bodi. Wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo wataendelea kupata mikopo yao kulingana na viwango walivyopangiwa awali.
1.1 Maombi yaliyopokelewa
Jumla ya maombi 58,037 yalikuwa yamepokelewa hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2014. Kati ya maombi hayo, jumla ya maombi 37,689 ni ya waombaji wa kiume na maombi 19,592 ni ya waombaji wa kike. Uchambuzi zaidi wa waombaji wa mikopo unaonyesha kuwa Waombaji wa kundi la diploma ya ualimu wa sayansi ni 480 (Me – 324, Ke – 156), Waombaji wa shahada ya uzamili/uzamivu (kwa vyuo vya ndani ya nchi) ni 276 (Me – 194, Ke – 82), Waombaji wa shahada ya kwanza (kwa vyuo vya ndani ya nchi) ni 56,922 (Me – 37,460, Ke – 19,462), Waombaji wa shahada ya uzamili/uzamivu (nje ya nchi) ni 126 (Me- 88, Ke – 38) na Waombaji wa shahada ya kwanza (nje ya nchi) ni 233 (Me – 141, Ke – 92).
1.2 Uchambuzi wa Maombi
Baada ya kufungwa rasmi kwa kipindi cha kupokea maombi ya mikopo, hatua inayoendelea kwa sasa ni uhakiki (verification) wa taarifa za waombaji, kwa kuzipitia nyaraka mbalimbali zilizoambatanishwa na waombaji mikopo ambazo ni cheti cha kuzaliwa, vyeti vya taaluma, vielelezo vya mdhamini, saini ya mwombaji na mdhamini wake na ushuhuda wa Mwanasheria au Hakimu kwamba vivuli vya nyaraka zilizowasilishwa kwenye Bodi ni halisi.
1.3 Upangaji wa mikopo
Mchakato wa uchambuzi na upangaji wa mikopo utakamilika baada ya majina ya wanafunzi waliodahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kujiunga na vyuo mbalimbali yanapowasilishwa rasmi kwenye Bodi ya Mikopo. Udahili wa wanafunzi unafanywa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa mfumo wa pamoja wa udahili (CAS) unaotumiwa na vyuo takribani vyote vya elimu ya juu nchini. Kwa vyuo ambavyo havimo katika mfumo wa pamoja wa udahili (CAS) hutuma TCU majina ya wanafunzi ambao vimewadahili ili waweze kuthibitishwa kabla ya kupatiwa mikopo. Taarifa za udahili ni muhimu katika zoezi la upangaji wa mikopo kwa kuwa zinatoa mwongozo wa gharama halisi za programu za mafunzo. Wanafunzi wanaostahili na waliotimiza masharti na vigezo vya ukopeshaji ndio hupangiwa mikopo kulingana na bajeti iliyotengwa na Serikali.
1.4 Kutangazwa kwa majina ya wanafunzi waliopata mikopo
Majina ya wanafunzi waliopata mikopo kulingana na udahili yatatangazwa kwenye tovuti ya Bodi na taarifa hiyo pia itatangazwa katika vyombo vya habari ili kuwataarifu wadau wote ikiwa ni pamoja na wanafunzi, vyuo vya elimu ya juu, wazazi na umma kwa ujumla. Nakala za majina ya wanafunzi waliopangiwa mikopo zitatumwa kwenye vyuo husika.
2.0 WANAFUNZI WA MASOMO YA STASHAHADA YA UALIMU
Kwa kutambua umuhimu wa masomo ya Sayansi na kukabiliana na upungufu
wa walimu wa masomo hayo katika ngazi ya shule za Msingi na Sekondari, mwaka huu serikali imetoa fursa ya mikopo kwa wanafunzi watakaojiunga na masomo ya Stashahada maalum ya Ualimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Wanafunzi wapatao 5,000 wanatarajiwa kujiunga na Stashahada hii maalum katika Chuo Kikuu cha Dodoma na wote watanufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
3.0 HITIMISHO
Kwa Taarifa hii, Bodi inapenda kuwataarifu wadau wote kuwa mchakato wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 unaendelea vema.
Aidha, Bodi inawasisitizia waombaji wa Mikopo, wazazi/walezi na umma kwa ujumla kutambua kuwa Mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya juu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Uchangiaji wa Elimu ya juu na hivyo iwapo kuna waombaji wanaoweza kujigharamia, wasiombe mikopo ili kutoa nafasi kwa wahitaji wengi zaidi kunufaika.
Imetolewa na:
KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU