Na Frank Mvungi
SERIKALI imejipanga kufanikisha mpango wa kitaifa wa urutubishaji vyakula na kusimamia usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwa lengo la kulinda afya ya walaji. Hayo yamesemwa na Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) bi Gaudensia Simwanza wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua Gaudensia amesema TFDA imeandaa kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula (Tanzania Food, Drugs and Cosmetics (food fortification) Regulations 2012). Alisema kuwa hatua nyingine ni kuandaa miongozo ya udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi ili kuwajengea uwezo wasindikaji kuweza kutekeleza matakwa ya kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula.
Akifafanua Gaudensia alisema kuwa upo mwongozo wa uhakiki wa ubora na usalama katika usindikaji wa mafuta ya kula yaliyoongezwa virutubishi na mwongozo wa uhakiki wa ubora na usalama katika usindikaji wa unga wa mahindi ulioongezwa virutubishi ili kuliunda afya ya mlaji.
Katika hatua nyingine Gaudensia alibainisha kuwa mwongozo wa usimamizi wa Kanuni za uongezaji virutubishi na mwongozo wa ukaguzi wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi ambapo pamoja na mambo mengine mwongozo huu umeainisha taratibu za kufuata katika udhibiti wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi muhimu katika chakula.
Vilevile alisisitiza kuwa utoaji wa mafunzo kwa wadau kuhusu uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi kama vile wataalamu kutoka katika viwanda ni muhimu kwa vile vinavyoongeza virutubishi kwenye vyakula.
Katika hatua nyingine, jukumu jinguine la TFDA ni kusambaza vitendea kazi vinavyotumika katika uhakiki na udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula na kusimamia utekelezaji wa kanuni za uongezaji wa virutubisho kwenye vyakula.
Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inafanya majaribio katika Halmashauri 6 za Mikoa ya Iringa, Kilolo, Iringa Vijijini, Njombe, Arusha, Karatu, Meru na Monduli ambapo kwa upande wa mafuta ya kula majaribio yanafanyika katika Mikoa ya Manyara, Singida na Dodoma.