Na Hassan Abbas
WATENDAJI wa Ofisi ya Rais-Usimamizi wa Utekelzaji wa Miradi ya Kipaumbele (PDB) inayosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) wametakiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika usimamizi na utekelezaji wa Mpango huo.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam leo Jumatatu na Naibu Mtendaji Mkuu wa PDB, Bw. Peniel Lyimo alipokuwa akifungua Mkutano wa Kwanza wa Watendaji Kutathmini Utekelezaji wa BRN.
“PDB ni taasisi ya Serikali yenye malengo ya kuhakikisha Mpango wa BRN unafanikiwa. Hivyo sisi watendaji tuliokabidhiwa jukumu hili tunapaswa kuwa chachu ya mabadiliko. Tunapaswa kuachana na mtindo wa kufanyakazi kwa mazoea,” alisema Bw. Lyimo.
Alisisitiza kuwa moja ya changamoto ambazo BRN imekumbana nazo katika mwaka mmoja wa utekelezaji ni suala la baaadhi ya watendaji kufanyakazi kwa mtindo wa kufanyakazi bila kujituma, kutojiwekea malengo na kutofuata vipimo vya ufanisi.
Watendaji wapya wa PDB walioajiriwa hivi karibuni na wale walioko kwenye Vitengo vya Utekelezaji kwenye Wizara mbalimbali wanakutana kwa mara ya kwanza katika kikao cha kutathmini mwaka mmoja wa utekelezaji wa Mpango huo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyofafanuliwa na Mkurugenzi wa Huduma za Utawala wa PDB, Bw. Maharage Chande na kutafakari mwaka mmoja wa BRN, watendaji hao pia watapatiwa uelewa kuhusu utendaji wa Serikali, utekelezaji wa BRN na kupatiwa mafunzo yanayohusu namna nchi nyingine hasa Malaysia zilivyofanikiwa katika kutekeleza miradi ya kipaumbele kama ya BRN.
PDB ilianzishwa Julai mosi mwaka jana chini ya Ofisi ya Rais kusimamia Mpango wa BRN wenye sekta sita za kipaumbele ambazo ni kilimo, maji, nishati, elimu, uchukuzi na ukusanyaji mapato.
Sekta mpya ya uboreshaji wa mazingira ya biashara (business environment) nayo imeingizwa rasmi katika BRN kuanzia Julai mosi mwaka huu huku sekta ya afya nayo ikiwa katika maandalizi ya kuingia BRN. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, siku ya alhamisi, Mtendaji Mkuu wa PDB, Bw. Omari Issa ataeleza mafanikio yaliyopatikana katika mwaka mmoja wa utekelezaji wa BRN.