ZIMBABWE imemtunukia Mtanzania, Katibu Mtendaji wa zamani wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita, Tuzo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la Zimbabwe kwa watu wachache sana duniani, tuzo ambayo pia inaambatana na zawadi ya dola za Marekani laki moja – sawa na shilingi milioni 160.
Rais Robert Gabriel Mugabe amemtunuku tuzo hiyo Brigedia Mbita kutokana na mchango wake wa kuitoa Zimbabwe katika minyororo ya ukoloni katika nafasi yake kama Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika ambayo aliingoza kwa miaka zaidi ya 20 tokea 1972 hadi 1994 wakati Afrika Kusini ilipofuta Ubaguzi wa Rangi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walioshuhudia tukio hilo kwenye Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe ambako viongozi hao wanakutana katika Mkutano wa 34 wa mwaka wa Viongozi wa SADC.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Taifa la Zimbabwe kutunuku tuzo hiyo kubwa na ya heshima zaidi kuliko nyingine yoyote ya Nishani ya Royal Order of Monomtapa kwa binadamu ambaye siyo Rais ama siyo Rais wa zamani. Nishani hiyo inapata jina lake kutoka kwa Mtawala wa eneo ambalo sasa ni Zimbabwe kabla ya wakoloni wa Kiingereza hawajaitawala nchi hiyo.
Maelezo ya Mzee Mbita yaliwasilishwa na Katibu Kiongozi wa Serikali ya Zimbabwe na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na Brigedia Mbita anakuwa binadamu wa sita kutunukiwa tuzo hiyo.
Watunukiwa wengine ambao mpaka sasa wamepata tuzo hiyo ni viongozi waanzilishi wa Umoja wa Nchi za Mstari wa Mbele katika Ukombozi wa Afrika (Frontline States) ni Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Augustino Neto wa Angola, Hayati Samora Machel wa Mozambique, Hayati Sir Seretse Khama wa Botswana na Rais Kenneth Kaunda wa Zambia.
Akikabidhi nishani hiyo, Rais Mugabe amemwelezea Mzee Mbita kama “kiongozi wa kijeshi na mkombozi ambaye alitoa mchango usiopimika na kuonyesha nia thabiti kwa ukombozi wa nchi zetu Kusini mwa Afrika. Ni mtu ambaye amesaidia jitihada za ukombozi katika kanda yetu na nje yake akitujengea misingi ya kuungwa mkono kijeshi, kisiasa na kidiplomasia.”
Ameongeza Rais Mugabe: “Huyu ndiye alikuwa kinara wa mapambano yetu yote kuanzia kwenye ustawi wetu, kupata sare za kivita, kuhakikisha safari zetu zinapangwa vizuri na kutupa ushauri wa kijeshi – huyo ndiye alikuwa Brigedia Komredi Hashim Mbita”.
Rais Mugabe ambaye ametunuku nishani hiyo kwa nafasi yake kama Rais wa Zimbabwe, Amirijeshi mkuu wa nchi hiyo ambaye anabeba nishani ya Grand Master of the Zimbabwe Order of Merit amesikitishwa na ukweli kuwa Mzee Mbita hakuweza kuhudhuria nafasi hiyo kwa sababu ya kudorora kwa afya yake. Badala yake nishani hiyo imepokelewa kutoka kwa Mzee Mugabe na Bi. Sheila Hashim Mbita, mtoto wa kwanza wa Brigedia Mbita ambaye ameishuku sana Zimbabwe na Rais Mugabe kwa uamuzi wao wa kumtunukia baba yake.
“Baba yangu ameshindwa kuhudhuria sherehe hii muhimu sana kwake, lakini alifurahi sana alipopewa habari za nishani hii. Mimi nikiwa mtoto wa kwanza katika familia namwakilisha baba yangu na familia yote,” amesema Bi. Sheila.
Ameongeza Bi. Sheila, “sisi kama familia tukiongozwa na baba yetu tunathamini sana nishani hii. Baba yangu aliingoza kwa muda mrefu ofisi ya Kamati ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika tokea mwaka 1972 hadi ilipofungwa mwaka 1994 baada ya Afrika Kusini kushinda siasa za Ubaguzi wa Rangi”.
Brigedia Hashim Mbita alikuwa Katibu Mtendaji wa tatu na wa mwisho wa Kamati ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika ambaye pia aliiongoza kamati hiyo kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine yoyote. Brigedia Mbita ni mtumishi wa umma mstaafu, ofisa wa jeshi, mwandishi wa habari na mwanasiasa ambaye kwa nyakati mbali mbali kabla ya kuwa Katibu mtendaji wa Kamati ya Ukombozi, alifanya kazi kama Ofisa Habari wa Mkoa, Ofisa Mkuu wa Habari wa Serikali, Mwandishi wa Habari wa Rais, Balozi.