Msichana wa Kitanzania Ashinda Insha ya SADC

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza mwanafunzi wa kidato cha nne Neema Steven Mtwanga(16) anayesoma katika shule ya sekondari Naboti Makambako,Njombe baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika utunzi wa insha katika shindano lililoandaliwa na Jumuiya ya uchumi ya maendeleo kusini mwa Afrika(SADC).Rais Kikwete alimpongeza mwanafunzi huyo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe ambapo mwanafunzi huyo aliandika insha inayohusu mabadiliko ya tabia nchi.

Rais Dk.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza mwanafunzi wa kidato cha nne Neema Steven Mtwanga(16) anayesoma katika shule ya sekondari Naboti Makambako,Njombe baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika utunzi wa insha katika shindano lililoandaliwa na Jumuiya ya uchumi ya maendeleo kusini mwa Afrika(SADC).Rais Kikwete alimpongeza mwanafunzi huyo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe ambapo mwanafunzi huyo aliandika insha inayohusu mabadiliko ya tabia nchi.

* SADC yaishukuru Tanzania kwa Ukombozi

MSICHANA Neema Steven Mtwanga, 16 ameibuka kinara katika Mashindano ya Utunzi wa Insha katika nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kushika nafasi ya kwanza miongoni mwa washindani 39 waliowania Tuzo ya Utunzi wa Insha hiyo kwa Mwaka 2014. Msichana Neema Steven Mtwanga, kutoka Shule ya Sekondari ya Naboti, Mkoa wa Njombe, ametunukiwa Tuzo ya ushindi huo katika Mkutano wa 34 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC ulioanza leo katika Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe.

Nafasi ya pili imeshikwa na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini Zimbabwe na nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi kutoka Shule ya Sekondari ya Etjendlovu katika Swaziland. Kwa ushindi huo, Neema Steven Mtwanga ambaye yuko kidato cha nne, amezawadiwa hundi ya dola za Marekani 1500 ambayo ni sawa na shilingi milioni 2.3 na amelipiwa gharama zote za kumwezesha kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC na kukabidhiwa zawadi hiyo. Aidha, Neema amepewa zawadi ya ipad kwa ajili ya matumizi yake ya teknolojia ya mawasiliano na habari.

Mashindano hayo ya Insha ya Mwaka 2014 yalianzishwa rasmi Oktoba, 2013 ambako washindani walitakiwa kuandika Insha kuhusu mada: “Climate Change is having adverse effect on the socio-economic development in the Region. What should the Education Sector do to mitigate the impact on the youth” – Mabadiliko ya Tabia Nchi yanaathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Kanda ya SADC. Nini Sekta ya Elimu ifanye kupunguza athari hizo kwa vijana?

Insha 39 zilipokelewa kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC ikiwa ni Insha tatu kwa kila nchi. Insha zilipokelewa kutoka Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe. Majaji wa kupitia na kuamua washindi wa Insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na Zimbabwe na walikutana mjini Gaborone, Botswana, Julai, mwaka huu kupitia Insha zote na kutoa uamuzi wa nani washindi. Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo wa SADC umepokea kwa furaha ushindi huo.

Wakati huo huo; Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeishukuru na kuipongeza tena Tanzania kwa mchango wake mkubwa na wa hali na mali uliofanikisha jitihada za mapambano ya ukombozi yaliyoleta uhuru kwa nchi za Kusini mwa Afrika. SADC imemshukuru na kumpongeza aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Afrika, Brigedia Hashim Mbita wa Tanzania, kwa mchango wake na uongozi wake wa mapambano ya ukombozi, iwe katika nyanja ya kuviwezesha vyama vya ukombozi kwa hali na mali, raslimali na ushauri.

Pongezi hizo kwa Tanzania zilitolewa usiku wa jana, Jumamosi, Agosti 16, 2014, na Kikao cha Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC – SADC Troika- kilichofanyika kwenye Hoteli ya Elephant Hills Resort, Victoria Falls, Zimbabwe, chini ya Uenyekiti wa Rais Hifikepunye Phohaba wa Namibia. Mkutano huo wa SADC Troika ulihudhuriwa na wanachama wa Asasi hiyo – nchi za Namibia, Lesotho na Tanzania. Nchi za Afrika Kusini, Madagascar na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilishiriki kama waalikwa maalum wa kikao hicho.

Akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya nwenzake, Rais Pohamba alisema: “Tunawashukuru wananchi wa Tanzania kwa mchango wao wa kiuchumi, kijeshi na kimkakati katika kuunga mkono kwa hali na mali jitihada za mapambano ya ukombozi wa nchi zetu.”
Aliongeza Rais Pohamba: “Sote tunaijua Tanzania, sote tunawajua Watanzania. Kwa pamoja walitoa jasho na damu na sisi wenyewe katika kutafuta ukombozi wa nchi zetu. Tutaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wao mkubwa na usiosahaulika kwa ustawi wa nchi zetu.”
Kuhusu Mzee Mbita, ambaye Ripoti yake ya shughuli za ukombozi ilitarajiwa kuwasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC, Rais Pohamba alisema: “Brigedia Mbita alifanya kazi mchana na usiku kufanikisha shughuli za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Tunamshukuru sana kwa uongozi wake na mchango wake mkubwa katika kuleta uhuru wa nchi zetu.”
Aliongeza: “Brigedia Mbita ni raia wa Tanzania na alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika iliyokuwa na makao makuu yake mjini Dar es Salaam. Alichapa kazi kweli kweli na chini ya uongozi wake, vyama vya ukombozi vilipata misaada ya hali na mali, misaada ya kiroho na ushauri wa kijeshi kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa mtu wa shughuli za jeshi.” Mzee Mbita aliongoza Kamati ya Ukombozi tokea mwaka 1974 hadi ilipomaliza shughuli zake.
Akizungumza kwa ufupi sana katika kikao hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alimpongeza sana Brigedia Mbita akisema kuwa alifanya kazi nzuri na kubwa na “tunampogeza kwa kazi nzuri sana ya kuandaa Ripoti hiyo.”
Ripoti hiyo inayojulikana kama Mradi wa Hashim Mbita iliongozwa na Meneja wa Mradi, Profesa Arnold Temu wa Tanzania na imechapishwa na Kampuni ya Mkuki na Nyota, pia ya Tanzania, ambayo Mtendaji Mkuu wake, Mzee Walter Bgoya ameandamana na mwakilishi wa Mzee Mbita kwenye mkutano huo.