Kenya Yafunga Safari za Sierra Leone na Liberia Kujikinga na Ebola

Moja ya ndege za Kenya Airways

Moja ya ndege za Kenya Airways

HATIMAYE Shirika la Ndege la Kenya Airways limesalimu amri na kukubali shinikizo la kusitisha safari za ndege kuelekea mataifa matatu yaliyoathirika kiasi kikubwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Titus Naikuni amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kupata ushauri wa Shirikisho la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya nchini Kenya hivyo wameamua kusimamisha safari zote za ndege kwenda Liberia na Sierra Leone.

Alisema utekelezaji wa hatua hiyo utaanza Agosti 19, 2014. Hata hivyo shirika hilo lilisema kuwa litaendelea na safari zake kuelekea nchi ya Nigeria. Alisema abiria wote ambao walikuwa wamenunua tiketi za kwenda mataifa hayo wanatarajiwa kurejeshewa fedha zao mara moja.

Juzi Shirika hilo la ndege lilitangaza kuwa linatarajia kusimamisha safari za ndege za kwenda nchi za Sierra Leone na Liberia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ulioyakumba baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi.

Awali uongozi wa shirika hilo kupitia, Mkurugenzi wa Afya ya Jamii, Nicholas Muraguri, alisema hakuna raia kutoka nchi zenye ebola atayeruhusiwa kuingia Kenya. Hivi karibuni WHO ilibainisha kuwa Kenya iko katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa Ebola kwa sababu ni nchi ambayo ina safari nyingi za ndege kwenda nchi za Afrika Magharibi. WHO piya ilisema makisio ya ugonjwa huo ulivotapakaa siyo kadiri ya hali halisi.
-BBC