NIDA Yaanza Usajili na Utambuzi Vitambulisho Mtwara

Ndugu Joseph Makani, Mkurugenzi Mifumo ya Komputa akisoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA, wakati wa uzinduzi wa kuanza kwa zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu mkoani Mtwara. Habari/Picha na Rose Mdami (NIDA)

Ndugu Joseph Makani, Mkurugenzi Mifumo ya Komputa akisoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA, wakati wa uzinduzi wa kuanza kwa zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu mkoani Mtwara. Habari/Picha na Rose Mdami (NIDA)


Na Mwandishi Maalum

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imezindua rasmi zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu kwa wananchi na wakazi wa Mkoa wa Mtwara, kabla ya kufikia hatua ya kutoa vitambulisho kwa wakazi hao. Kwa mujibu wa taarifa kutoka NIDA zoezi hilo la awali litadumu kwa siku 14 kuanzia Jumatatu ya Agosti 18, 2014.

Akizungumza katika sherehe fupi ya uzinduzi wa zoezi hilo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho, Joseph Makani amesema kuanza kwa zoezi hilo Mtwara ni utekelezaji wa mpango wa Usajili wa wananchi na wakazi waishio kihalali nchini wenye lengo la kuwapatia vitambulisho vya Taifa Raia, Wageni na Wakimbizi baada ya zoezi kama hilo kukamilika wa wananchi wa Tanzania Zanzibar, mikoa ya Dar-es-salaam, Pwani na sasa Mtwara.

Alisema ufanisi wa zoezi hilo unategemea sana ushirikiano toka kwa viongozi katika serikali, vyama vya siasa na viongozi wa Dini ambao walikuwepo kushuhudia tukio hili.

Naye mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala Mkoa ndugu Jehasen Bukwali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ameahidi kutoa ushirikiano na kusimamia kwa dhati zoezi hilo kufanyika katika mkoa wa Mtwara, huku akiwataka viongozi katika ngazi zote kushiriki kikamilifu katika kufanikisha zoezi la Usajili ambalo linamatokea makubwa katika ustawi na maendeleo ya Taifa.

Aidha amewaasa wananchi na wanasiasa kutohusisha zoezi hilo la Siasa, kwani vitambulisho vya taifa havihusiani na itikadi za chama chochote, na haki ya kila Mtanzania kusajiliwa na kupata haki yake msingi kikatiba. Ufunguzi huo uliwakilishwa na viongozi katika ngazi za juu Mkoa, na Wilaya zikiwemo kamati za Ulinzi na Usalama.