MBUNGE wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasini amewataka wakazi wa Wilaya ya Rombo kuweka pembeni itikadi zao za kisiasa na badala yake kushirikiana na viongozi waliochaguliwa ili waweze kuleta maendeleo.
Mbunge aliyasema hayo wakati alipokuwa akihutubia wakazi wa Kata ya Mrao Keryo, Tarafa ya Mashati Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro. Amewataka wananchi kuacha tabia ya kukaa vilabuni na kunywa pombe muda wote kwani kwa tabia hiyo imewafanya watu wengi kusahau familia zao kutokana na ulevi.
“Ndugu zangu lazima niliseme hili, wilaya yetu imekua ya kwanza kitaifa kwa kuongoza kwa unywaji wa pombe za kienyeji, lazima tuyaache haya ambayo hayana tija na tufanye kazi kwa nguvu zote,” alisema mbunge na kuongeza,” alisema.
“…Utengenezaji wa pombe hizi hauzingatii ubora wa kiafya, umevunja ndoa nyingi…umepunguza nguvu kazi sasa ukimwona kijana wa miaka 18 hivi sasa amezeeka zaidi ya mzee wa miaka sabini…ndugu zangu tuyaache haya tufanye kazi” alisema Selasini.
Aidha katika hatua nyingine Selasini aliahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni mbili kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa zahanati ya kjijii hicho.