Na Magreth Kinabo na Rose Masaka
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta amewahakikishia Watanzania kwamba Katiba Mpya itakayopatikana itakuwa imezingatia matakwa ya makundi mbalimbali. Sitta aliyataja makundi hayo kuwa ni wafugaji, wakulima, wavuvi na wasanii. Huku akisema Katiba Mpya itakayopatikana itakuwa ni bora kuliko ya iliyopo sasa.
Kauli hiyo ilitolewa na Sitta wakati akizungumza na wafugaji wapato 44 kutoka mikoa mbalimbali, ambao waliongozwa na Mwenyekiti wa ujumbe huo, Huruma Ole Kalaita na Mlezi wao, ambaye mjumbe wa Bunge hilo na Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi (CHADEMA).
“Tunaamini ni wakati wa Katiba Mpya…lazima iweze kupatikana. Itakayozingatia Sheria bora na maslahi ya makundi mbalimbali yatapatikana. Utungaji wa Katiba ni suala la wananchi kutanguliza suala la muundo wa Serikali si haki. Ni muhimu kutanguliza haki za raia. Kinachotangulia ni haki za raia wetu na makundi mbalimbali,” alisisitiza Sitta.
Aidha Mhe. Sitta aliwakikishia wafugaji hao, kwamba Bunge hilo “liko hapa kisheria kwa kanuni zake linaendelea na wale wanaopiga kelele hawalitakii mema taifa letu kwa sababu demokrasia yoyote ni kupata kura ya walio wengiu,” alisema.
Kwa upande wake Mlezi wa wafugaji hao, Shibuda alimpongeza Sitta kwa jitihada zake za kuendeleza vikao vya Bunge hilo, ambapo pia alimsihii kuwa asikatishwe tamaa kwa dhamira yake njema ya kuendelea kuongoza vikao vya Bunge hilo. Akizungumzia kuhusu masuala ya wafugaji hao na wakulima wa zao la pamba nchini, alisema kuwa wako pamoja naye.
“Hivi Serikali tatu au mbili inatiririsha nini kwa wakulima na wafugaji. Tunataka viongozi wa kukabiliana na matatizo ya wananchi,” alisisitiza Shibuda.
Kwa upande Mwenyekiti wa wafugaji hao, Kalaita alipendekeza Katiba Mpya, itamke matumizi bora ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji. Makamu wa Mwenyekiti wa wafugaji hao, Kasundwa Wamalwa kutoka Kanda ya Magharibi akisoma mapaendekezo ya risala yao waliyoiwasilisha kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Sitta, ambapo walipendekeza Katiba Mpya itambue wafugaji wa asili.
Aidha Makamu Mwenyekiti huyo aliwataka wajumbe wa Bunge hilo, kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu wakati wanapoendelea na mchakato huo. Miongoni mwa makundi mengine waliofika katika ofisi za Bunge mjini Dodoma ni Jukwaa la Katiba (JUWAKATA) na Jukwaa la Wahariri.
Wakati huo huo; UKAWA waombwa kukubali maoni ya watanzania walio wengi ya kuheshimu pesa za walipa kodi kwa kurudi bungeni na kupingana kwa hoja kwani hoja zao zikiwa za huakika hazitapingwa bali kanuni na taratibu zinazoendesha bunge zitafuatwa badala ya kuendelea kulalamika katika majukwaa ya kisiasa. Kauli hiyo imetolewa na balozi wa amani Tanzania Risasi Mwaulanga alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa habari maelezo leo jijijni Dar es Salaam.
“Nawaomba UKAWA warudi bungeni ili tuweze kupata katiba mpya itayoyokidhi changamoto za watanzania wote na sio masuala ya vyama vya kisiasa na maslahi binafsi kwani vyama hiyvo vinaweza kutoweka wakati wowote na nchi ikabaki palepale”.Alisema Mwaulanga.
Aidha Mwaulanga anaiomba iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya jaji Warioba, viongozi wa dini, na asasi za kiraia kuendelea na jitihada za kuitaka UKAWA kurejea Bungeni ili kurahisisisha upatikanaji wa Katiba mpya yenye maslahi mapana kwa ummma kuliko ya kisiasa. Balozi huyo wa amani amesema kuwa kauli za vitisho na uvunjifu wa amani unapaswa kupigiwa kelele na kulaniwa na kila mwanademokrasia duniani katika kipindi hiki cha kuandaa Katiba mpya ili wajumbe waweze kuwa huru wakati wa kutoa maoni.
Tanzania ni nchi ya amani,umoja, upendo na maelewano na siyo nchi ya vita,chuki na mafarakano hivyo watanzania tunapaswa kutambua ni Katiba gani tunayoitaka na kuwa na mtazamo sahihi na maamuzi bora.