Na Eleuteri Mangi – MAELEZO
SERIKALI imetenga fungu la fedha ambalo litagawiwa kwenye vituo vyote vinavyotoa ushauri nasaha na kurekebisha watoto walio chini ya umri wa miaka 18 (mahabusu) zilizopo chini ya Idara ya Ustawi wa jamii nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja kufuatia habari iliyochapishwa na gazeti la Majira toleo Na. 7524 Vol.II/5624 la Jumatano Agosti 13, mwaka huu yenye kichwa cha habari “Mahabusu ya watoto yadaiwa mil. 1/=”.
“Ni kweli tatizo hilo lipo ndio maana Serikali imetenga fedha tayari ambazo zitagawiwa kwenye vituo vyote nchi nzima,” alisema Mwamwaja. Mwamwaja alisisitiza kuwa deni hilo litalipwa kweye mahabusi hiyo iliyoko Tanga.
Mahabusi hiyo ni miongoni mwa vituo kadhaa vilivyo chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii ndani ya Wizara ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Matumizi ya fedha hizo ni pamoja na kushughulikia tatizo la maji na uhaba wa chakula kituoni hapo ili kuendelea kutoa huduma stahiki kwa watoto hao na kufikia lengo la kuwarekebisha tabia zao ili wawe raia wema nchini.
Aidha, Mwamwaja aliongeza kuwa fedha zilizotengwa si za Mkoa wa Tanga tu bali ni kwa ajili ya vituo vya nchi nzima zikiwemo makambi ya wazee wasiojiweza, mahabusi za watoto na kambi za kutibu wagonjwa wa ukoma.