UKAWA Wamtaka Rais Kikwete Kusitisha Bunge la Katiba

Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe  akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.  Wanaomfuatia ni wenyeviti wenza wa umoja huo James Mbatia (katikati) na Profesa Ibrahimu Lipumba.

Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe  akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.  Wanaomfuatia ni wenyeviti wenza wa umoja huo James Mbatia (katikati) na Profesa Ibrahimu Lipumba.

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma na iwapo hatafanya hivyo utaongoza maandamano nchi nzima.

Umoja huo pia umeeleza kuwa kuendelea kwa Bunge hilo ni sawa na kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya, kuiweka nchi rehani, kufuja fedha za walipakodi, kuwahadaa Watanzania kwa kupitisha Katiba isiyotokana na maoni yao, huku kanuni zikibadilishwa na kuingizwa mambo ya Tanganyika katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kadhalika, umemtaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha za Bunge hilo kwa maelezo kuwa zinatumika bila maelezo sahihi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) akiwa na wenyeviti wenzake, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), alisema hawatataja muda lakini wanataka jambo hilo lifanyike haraka iwezekanavyo.

“Iwapo Rais Kikwete hatatumia mamlaka yake kusitisha Bunge na kukubali liendelee kinyume na matakwa ya wananchi, Ukawa tutawaongoza Watanzania kupaza sauti kupinga najisi inayotiwa kwenye maoni yao, kupitia maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima,” alisema Mbatia.

Akizungumzia iwapo Rais anayo mamlaka ya kusitisha vikao vya Bunge hilo, Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema anaweza kufanya hivyo kwa kutumia dhamana ya uongozi aliyonayo, lakini kisheria hawezi kutokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kutokuwa na ibara inayompa mamlaka hayo.

“Rais ni Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa nchi na Serikali. Majukumu hayo ndiyo yanayomfanya awe na uwezo wa kusitisha shughuli za Bunge hilo, hasa akiona theluthi mbili ya wajumbe kutoka kila upande kwa ajili ya kufanya uamuzi haitapatikana.”

Aprili 16, mwaka huu wajumbe wanaotokana na vyama vya siasa vinavyounda Ukawa na baadhi kutoka Kundi la 201, walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa katika rasimu.

Mbatia alisema Ukawa imechukua uamuzi wa kuandamana kutokana na wajumbe wa CCM pamoja na wengine 166 walioteuliwa kupitia kundi la wajumbe 201, kuendelea na vikao vya Bunge hilo na kuingiza mambo yao katika Rasimu ya Katiba, huku wakilipwa fedha za walipakodi.

“Mambo wanayoyajadili na kuyachomeka kinyemela kwenye rasimu kama ardhi, elimu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo na serikali za mitaa ni masuala yanayopaswa kuandikwa kwa kina ndani ya Katiba ya Tanganyika siyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Zanzibar walijadili wenyewe mambo yao ya ndani na kutengeneza Katiba yao, hivyo hatuoni mantiki ya wajumbe kutoka Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya Tanganyika. Bunge la Katiba halina sifa za kujadili mambo yasiyo ya muungano. Hii inaonyesha CCM wamelewa madaraka.”

Alisema ili Bunge hilo lipate uhalali wa kuendelea yanatakiwa kufanyika maridhiano ya pande zote zinazovutana na kusisitiza kuwa kinachoendelea sasa kinatokana na kukosekana kwa uongozi wa kisiasa.

“Wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema kuwa suala la muundo wa serikali lilitakiwa kupigiwa kura, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samwel Sitta anaendelea kuongoza Bunge kama mchakato ni mali yake binafsi. Baadhi ya viongozi wa chama hicho wanataka mchakato usitishwe, wengine wanataka uendelee,” alisema.

Mbatia alisema Ukawa inashangazwa na Rais Kikwete kwa kitendo chake cha kufanya ziara ya kutembelea ranchi binafsi ya kufugia wanyama ya aliyekuwa Rais wa Marekani, George Bush wakati nchi ikiwa katika sintofahamu ya mchakato wa kupata Katiba Mpya huku watu wa kada mbalimbali wakitaka mchakato usitishwe.

Profesa Lipumba alisema: “Wapo wanaosema kuwa Ukawa tumegawanyika. Hilo siyo kweli kwa sababu waliotusaliti na kuhudhuria vikao vya Bunge hata asilimia tano hawafiki. Zaidi ya asilimia 95 hatujakwenda bungeni,” alisema.

Alisema kuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alitenga masuala ya ardhi, maliasili na Serikali za Mitaa ili yaingizwe katika Katiba ya Tanganyika, hivyo kuyajadili mambo hayo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano si sahihi. Mbowe alisema: “Viongozi wanaiacha nchi ijiendeshe yenyewe. Ni kama ndege ambayo rubani yupo lakini ameweka ‘auto pilot’, yaani wameiruhusu ndege ijiendeshe yenyewe.”

CAG achunguze
Kuhusu suala la ukaguzi wa hesabu, Mbatia alisema katika vikao vya Bunge la Bajeti, baadhi ya wabunge walihoji zinakopatikana fedha za kuendesha Bunge la Katiba na kusema kutokana na hali hiyo, ni vyema CAG akachunguza kwa undani suala hilo.

Hoja kutaka Bunge hilo lisitishwe inaungwa mkono na makundi mbalimbali pamoja na baadhi ya wabunge wa CCM, akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba (Iramba-Magharibi) aliyesema likiendelea bila uhakika wa kupata akidi ya uamuzi itakuwa ni kupoteza zaidi ya Sh20 bilioni za walipa kodi na wananchi hawataelewa.

Hata hivyo, uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa vikao hivyo ambavyo awali vilifanyika kwa siku 67, vitaendelea kwa siku 60 za kazi zilizoongezwa na Rais Jakaya Kikwete, bila kuhusisha siku za Jumamosi na Jumapili ambazo zinaongeza muda wa wajumbe kukaa Dodoma kuwa 84.

CHANZO: Mwananchi