MJUMBE wa Baraza la Uendeshaji la UNESCO linalosimamia ukuzaji wa utamaduni, Dk. Mary Mbiro Khimulu amesema machafuko na mauaji hayana uhusiano wowote na dini ambayo ni ya kweli. Ametoa kauli hiyo Agosti 11, 2014 wakati akishiriki mjadala wa jinsi ambavyo bara la Afrika linakabiliana na migogoro inayotokea barani humo kwenye mkutano wa Dunia unaojadili masuala ya Amani, Usalama na Maendeleo jijini Seoul, Korea Kusini.
Dk. Khimulu ambaye ni raia wa Kenya, alisema: “Dini ya kweli haiwezi kuruhusu umwagaji wa damu, hakuna dini ya kweli inayochochea mauaji wala kuruhusu mapigano. Ninawasihi wote mliopo hapa, msiruhusu dini zenu zitumike kufanya mambo mabaya.”
Dk. Khimulu alisema ili kuepuka migogoro ya dini, anashauri diplomasia ya utamaduni (cultural diplomacy) itumike kuleta amani, usalama na maendeleo barani Afrika. “Kwa kuitumia diplomasia ya utamaduni, tuangalie ni kwa njia gani mijumuiko ya pamoja ya kidini (inter-faith communities) inaweza kutumika kuleta amani, upendo na mshikamano kwenye jamii tunazoishi,” alisema.
Vilevile, Dk. Khimulu alisema kwa kutumia diplomasia ya utamaduni tunaweza kuvunja chuki na kuleta mshikamano na umoja miongoni mwa watu wetu, watu wakatembeleana kupitia michezo, nyimbo au matamasha, na wakajenga mahusiano ya kuheshimiana kidugu.
Alisema kwa kuwa vita huanzia akilini mwa mwanadamu, ni humo humo ambamo mawazo ya kuacha mapigano ama machafuko yanapaswa kuingizwa. “Kwa hiyo tuitumie diplomasia ya utamaduni kama njia pekee ya kujenga mahusiano ya karibu kwenye jamii zetu na itusaidie kufikia malengo yetu ya kupata amani na usalama kwa watu wetu,”aliongeza.
Mapema, Balozi wa Kudumu wa AU kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Antonio Tete alisema wakati Umoja wa Afrika unaanzishwa mwaka 1963, baadhi ya wakuu wa nchi walikuwa na ndoto ya kuwa na jeshi moja barani Afrika ambalo lingekuwa na kazi ya kukabili migogoro yote barani humo.
“Kutokana na mabadiliko ya wakati na kadri muda ulivyosonga mbele, matarajio yao hayakutumia. Viliundwa vikosi vya muda navyo havikudumu. Tumeshuhudia miaka ya 90 kwenye migogoro ya Rwanda na ya Somalia. Hakuna jeshi lilipelekwa wala hakuna askari waliokuja kutoka nje,” alisema.
Alisema Umoja wa Afrika unakabiliwa na changamoto ya kukosa fedha za kujiendesha kubwa likiwa ni la kusimamia amani na usalama wa nchi wanachama. “Tunayo programu ya ulinzi na usalama lakini asilimia 90 ya mpango huu inachangiwa na wafadhili kutoka nje ya nchi. Hii siyo kazi rahisi… huwezi kujiendesha namna hii,” alisema.
Changamoto nyingine aliyoitaja ni kuwepo kwa vikund vya kigaidi. “Hawa wanaendesha mambo yao tofauti na kwa teknolojia ya hali ya juu, hata ungekuwa na jeshi la aina gani si rahisi kuwashinda… huwezi kutumia njia za kawaida za kupambana na uhalifu unapokabiliana na makundi ya aina hii,” alisema.
Katika hatua nyingine, Balozi Tete aliwaomba baadhi ya washiriki wafikirie kuwekeza barani Afrika kama njia mojawapo ya kuleta amani ya kudumu katika bara hilo. “Kwa muda mrefu bara hili limetumika kama chanzo cha malighafi kwa viwanda vya Ulaya na Amerika. Ni wakati sasa tubadili muelekeo na tufikirie kuwekeza katika bara hili kwani kwa kufanya hivyo mtasaidia kutengeneza ajira nyingi kwa vijana wa Afrika kupitia viwanda ambavyo mtavijenga.”
“Kukiwa na ajira za kutosha, mtaleta maendeleo na mtaleta amani kwa vile mtapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro na machafuko yanayotokana na kugombea rasilmali haba zilizopo,” alisema.