Rais Kikwete Aeleza Siri ya Utulivu na Amani Tanzania

Rais Jakaya Kikwete akizungumza.

Rais Jakaya Kikwete akizungumza.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa nchi tulivu, yenye umoja na amani kwa sababu ya sera nzuri ambazo zilianzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na ambazo zimeendelezwa na viongozi wakuu ambao walimfuatia Mwalimu.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania imefanikiwa kudumisha umoja, mshikamano na utulivu kwa sababu ya kuwa na sera zenye kujumuisha kila mmoja bila kubagua Mtanzania yoyote kwa misingi ya kabila, dini, rangi, imani zake na mahali atokapo.

Rais Kikwete ametoa ufafanuzi huo, Agosti 8, 2014, wakati alipozungumza mjini Houston na taasisi ya ushauri na utafiti ya Stratfor yenye makao makuu yake katika Jimbo la Texas, Marekani. Akijibu swali kuhusu nini hasa siri ya utulivu, amani na ushikamano wa Watanzania, Rais Kikwete amesema: “Tumekuwa na changamoto zetu nyingi kama taifa lakini tumekabiliana nazo vizuri na nchi imebakia salama, tulivu na yenye umoja. Tumekuwa na sera bora za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Tumetunga sera za kumnufaisha kila mtu bila kumbagua mtu yoyote kwa sababu zozote zile.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Sera hizo zilianzishwa na Baba wa Taifa na sisi viongozi tuliofuatia tumeziendeleza sera hizo. Hakuna ubaguzi wa rangi, ama kabila, ama dini, ama sehemu atokapo mtu. Na ili kuhakikisha kuwa sera hizi zinaendelea kuwa na maana tumefungua upeo na nafasi ya kisiasa. Tuna demokrasia inayofanya kazi, Tuna uhuru wa kushirikiana na uhuru wa habari.”

Amesisitiza Rais Kikwete ”Kama wewe ni kiongozi ambaye amefungua milango ya demokrasia, huwaonei watu wako wala kuwaua na kuwatesa, kama umefungua milango ya nchi kuwa na utulivu kwa nini nchi isiwe na amani na utulivu.”

Rais Kikwete pia ameishukuru Marekani kwa misaada yake mingi kwa Tanzania ikiwemo misaada ya kupambana na ukimwi na malaria, ya ujenzi wa miundombinu ya MCC, ya kilimo ya Feed the Future na Sacgot, uchapishaji wa vitabu vya kufundishia katika shule za sekondari.

“Sasa tunaingia katika eneo jipya la biashara na uwekezaji kufuatia mkutano wa Washington ambako viongozi wa Afrika walikutana na Rais Barack Obama kuzungumzia aina mpya ya ushirikiano kati ya sehemu hizi mbili”.