NDEGE iliyokuwa na abiria 40 imeanguka mjini Tehran nchini Iran na kuuwa abiria wote. Runinga ya taifa la Iran imesema abiria wote wanaaminika wamefariki. Taarifa zaidi zinasema ndege hiyo ya kampuni ya Taban Air imeripotiwa kuanguka katika makazi ya watu muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa Mehrabad Maghribi mwa mji wa Tehran.
Ndege hiyo inayojulikana kama Iran 141 ilitengezwa nchini Iran kupitia teknologia ya Ukraine. Uchunguzi umeanzishwa kuangalia ni nini chanzo kilichosababisha ajali hiyo.
Iran imekuwa ikikabiliwa na matukio ya ajali kama hizo katika siku za hivi karibuni kutokana na ndege zake zilizozeeka mbali na marekebisho mabaya inazozifanyia. Marekani imesema kuwa imetekeleza mashambulizi zaidi kazkazini mwa Iraq dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji wa Jihad.
Wakati huo huo; taarifa kutoka Pentagon zimesema kuwa ndege za Marekani pamoja na zile zisizo na rubani ziliharibu magari ya kijeshi ya wanamgambo hao likiwemo lile lilokuwa likiwashambulia raia wa Yazidi ambao wamekimbilia hifadhi katika mlima Sinjar.
Awali Rais Obama alisema kupitia washirika wake wa ulaya pamoja na wanajeshi wa Iraq watawakabili wanamgambo ambao wameuzunguka mlima huo. Hatahivyo ameonya kuwa kampeni hiyo ya kijeshi itachukua miezi kadhaa na kwamba itachukua mda kwa jeshi la Iraq kujikusanya ili kutoa upinzani mkali dhidi ya wanamgambo hao.
Hata hivyo ndege za kijeshi za Marekani na zile za Uingereza zimeendelea kuangusha misaada kwa raia waliokwama katika Mlima Sinjar nchini Iraq, ijapokuwa viongozi wa mataifa hayo mawili wamekubaliana kwamba hatua hiyo sio suluhu ya kudumu. Wamesema kuwa lazima njia ya kuwaondoa raia hao hadi katika eneo lililo salama itafutwe ili kuzuia mauaji ya kimbari.
Mfanyikazi mmoja wa shirika la Amnesty International kaskazini mwa Iraq, Donatella Rovera amesema maelfu ya raia kaskazini na magharibi mwa mlima huo wamekimbia makazi yao, lakini wengi zaidi katika eneo la kusini la mlima huo hawana mahala pa kwenda. Amesema kuwa wale waliotoroka wako katika hali mbaya baada ya kukaa siku sita bila chakula na maji kidogo.
-BBC