Mama Kikwete Ataja Sababu za Vifo vya Wanawake…!

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda – Washington

KUTOKUWA na uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, upungufu wa huduma za afya na vitendea kazi, utungaji wa sera zisizo rafiki pamoja na ukosefu wa takwimu za magonjwa ni moja ya sababu zinazosababisha wanawake wengi kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wake wa marais wa Afrika waliohudhuria hafla fupi ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na kituo cha Marais wa Afrika (African Presidential Centre) cha chuo kikuu cha Boston iliyofanyika mjini Washington.

Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kwa kiasi kikubwa kuna mahusiano kati ya ugonjwa wa Ukimwi na Saratani ya mlango wa kizazi ambao kama mgonjwa atapata matibabu mapema atapona lakini kutokana na uelewa mdogo baadhi ya wanawake wanapoteza maisha.
 
“Kutokana na utaalamu uliopo sasa ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi unazuilika na kutibika lakini bado kuna uelewa mdogo katika jamii kuhusu uhusiano uliopo kati ya ugonjwa huu na ule wa Ukimwi; kama zitapatikana fedha za kutosha asasi zisizo za kiserikali ambao ni wawezeshashi wataweza kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na magonjwa haya”, alisema Mama Kikwete.
 
Akiongelea kuhusu maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi Mama Kikwete alisema ugonjwa huo unasababisha vifo vya watu wengi lakini bado kuna magonjwa mengine ambayo ni tishio nchini kama Malaria na Kifua kikuu ambayo nayo yanaua watu wengi.
 
Alisema, “Ugonjwa wa Ukimwi unasababisha vifo vya wanawake wengi nchini kwa upande wa vijana watoto wa kike wanaathirika zaidi ukilinganisha na watoto wa kiume na kwa watu wazima wanawake wengi wanapata maambukizi zaidi ukilinganisha na wanaume.
 
“Maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi yamepungua kutoka asilimia 7 kwa mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2012 kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar maambukizi ni asilimia 0.6% kwa miaka yote hiyo”.
 
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema vituo vya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) vimeongezeka kwa sababu vituo vilivyokuwa vinatoa huduma ya uzazi na watoto wachanga hivi sasa vinatoa huduma ya upimaji wa maambukizi ya VVU lakini bado jitihada kubwa zaidi zinahitajika kufanyika ili kuwe na vituo vingi vya kutoa huduma hiyo.
 
Kwa upande wa vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 147 kwa kila vizazi hai 1000 kwa mwaka 1999 hadi kufikia vifo 81 kwa mwaka 2010. Vifo vya watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 99 na kufikia 51 kwa kila vizazi hai 1000 ingawa tatizo limepungua hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa ili kuimarisha afya ya watoto.
 
Kuhusu vifo vya kina mama wajawazito alisema vimepungua kutoka 578 kati ya vizazi hai 100,000 mwaka 1996 hadi kufikia 454 kati ya vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2010 hii inatokana na jamii kuwa na uelewa juu ya umuhimu wa mwanamke kuhudhuria kliniki mapema pindi apatapo ujauzito na kujifungulia katika vituo vya afya.
 
Mama Kikwete alisema, “Vifo vingi vya kina mama wajawazito vinatokana na kutofuata uzazi wa mpango na uchumi mdogo wa wanawake, utoaji wa mimba usio salama, kuvunja damu nyingi wakati wa kujifungua, kifafa cha mimba, kushindwa kujifungua, uhaba wa huduma za haraka za uzazi na huduma za mtoto mchanga na uhaba wa watoa huduma za afya waliobobea,”.
 
Aliendelea kusema vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua vinahusiana na afya ya mama wakati wa ujauzito, hali ya kujifungua na jinsi ya kumjali mtoto wakati wa kujifungua. Mwanamke atakayejifungua mtoto akiwa na umri mdogo atakuwa na watoto wengi ambao umri wao haujapishana hayo  yote yana madhara kwa afya ya mama na mtoto .
 
“Ili kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga, ugonjwa wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi na Ukimwi hasa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto Taasisi ya WAMA inafanya kazi ya uraghibishi kwa kutoa vifaa tiba na elimu ya uzazi kwa vijana. Tunawakaribisha ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja ya kuokoa maisha ya mama na mtoto wa Tanzania”, alisisitiza Mama Kikwete.
 
Akiwakaribisha wake hao wa Marais Mkurugenzi wa Kituo cha Marais wa Afrika Balozi Charles  Stith aliwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya katika nchi zao ya kujali afya ya mama na mtoto na kuwataka waendee na kazi hiyo bila ya kukata tamaa kwani wao kama viongozi wanahitajika katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii inayowazunguka.
 
Balozi Stith alisema kituo chake kinatambua mchango wao na kazi wanayoifanya hasa katika kushughulikia afya ya mama na mtoto na upatikanaji wa elimu ya mtoto wa kike na kuhahidi kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana nao ili waweze kutekeleza majukumu yao.
 
Mama Kikwete anauhudhuria mkutano wa wake wa Marais wa Afrika ulioandaliwa na Mke wa Rais wa Marekani Mama Michelle Obama kwa kushirikiana na Taasisi ya George W. Bush ambao unajadili matatizo ya vifo vya kina mama wajawazito na watoto, ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti na elimu ya mtoto wa kike.