Wanawake wa kitanzania waishio Ughaibuni wamewatakiwa kuondoa tofauti zao za mitizamo, maoni, dini na makabila bali wapendane, kuaminiana na kushirikiana ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na hivyo kujiletea maendeleo.
Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanawake wafanya biashara na wajasiriamali kutoka majimbo ya Washington DC, Wilaya ya Colombia, Maryland na Virginia katika ukumbi wa mikutano wa ubalozi wa Tanzania uliopo mjini humo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema mwanamke wa kiafrika anazo changamoto nyingi za kihistoria na kimfumo ambazo humkwaza katika juhudi zake za kujiendeleza na kuendeleza wanawake wengine hivyo inapotokea wanawake wenzie wanamuandama na kumpiga vita jambo hilo humvunja nguvu na kumkatisha tamaa.
“Katika mazingira ya sasa ndani ya jamii nyingi tatizo hili lipo, wanawake wanaendelea kupigana vita, kushambuliana kwa maneno na kashfa mbalimbali matokeo yake ni kupungua kwa fursa ya kukutana na kutokuaminiana. Acheni kufanya hivyo kwani kila mmoja wenu anamuhitaji mwenzie na nchi yenu inawahitaji nyote ili muweze kuwasaidia wenzenu mliowaacha nyumbani.
Kwa mfano matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo mara nyingi yameharibika ushirikiano baina ya wanawake wa Tanzania hususani vijana na wanawake wa umri wa kati inafikia hatua mtu anapohudhuria sherehe au mijumuiko hajui ni picha na ujumbe gani utakaosambazwa kumhusu yeye”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa malezi ya watoto aliwataka kuwalea katika maadili mema yanayoendana na utamaduni wa mtanzania kwani hivi sasa kutokana na utandawazi baadhi ya wanawake wamesahau jukumu ya kuwalea watoto wao na kuwaachia wadada wa kazi kitendo ambacho kinasababisha watoto kuwa na mienendo mibaya.
Mama Kikwete alisema, “Hivi sasa jamii imekuwa na tabia ya kulalamika kuwa tabia za watoto si nzuri lakini ukiangalia chanzo ni wazazi wenyewe hasa kina mama ambao wamesahau wajibu wao wa malezi na kuwaachia wadada wa kazi. Wewe kama mzazi unatakiwa kuwa mfano wa kuigwa ili mtoto wako akue katika malezi na maadili yanayofaa”.
Mama Kikwete pia aliwataka wanawake hao kushiriki katika chaguzi mbalimbali ili waweze kufika katika ngazi ya maamuzi pia wakipata fursa wahakikishe wanakuwa mfano mwema kwa wanawake wengine na kuwa kichocheo cha kuhamasisha wenzao kwa kuonesha kwamba mwanamke anaweza na anapopata nafasi ya uongozi jamii hunufaika.
Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwashukuru wanawake hao kwa tuzo waliyompatia na kusema kwamba tuzo hiyo ni ya wanawake wote wa Tanzania ambao kwa ushirikiano wao wameweza kupata mafanikio kadhaa katika jamii yao.
Alimalizia kwa kuwaomba waweze kushirikiana na kufanya kazi pamoja na Taasisi ya WAMA ya kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania kwa manufaa ya nchi yao.
Akisoma hotuba ya ukaribisho kwa niaba ya Balozi Liberata Mulamula Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani Lilian Munanka alisema wanawake waisho ughaibuni nchini humo wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za maendeleo na uchumi sio tu kwa ajili yao na familia zao bali pia kwa ajili ya jamii nzima.
Alisema wanawake hao wamekuwa wakihakikisha kuwa nchini Tanzania wanawake wenzao waliokosa fursa ya kupata huduma za kijamii nao wanazipata zikiwemo huduma za afya na upatikanaji wa maji safi ya visima.
Kwa upande wa msoma risara ya wanawake hao Harrieth Shangarai alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania na kuwataka watu wengine kuiga mfano wake.
Shangarai alisema katika jumuia yao kuna wanawake wanaofanya kazi ya kuwasaidia wanawake na watoto walioko Tanzania na kuwaomba wanawake wenzao kutumia muda wao ili waweze kuelimishana na kuisaidia jamii yenye matatizo hasa kina mama wenye ugonjwa wa Fistula.
Wanawake hao walimpatia Mama Kikwete tuzo kutokana na kazi anayoifanya ya kuwasaidia wanawake na watoto wa kitanzania ili waweze kupata elimu bora na huduma nyingine sahihi za maisha katika jamii na kujenga familia zenye afya njema na kuleta maendeleo ya taifa.