Rais Kikwete Ataja Sifa Pekee ya Uwekezaji Tanzania

President Jakaya Mrisho Kikwete enjoys a light moment with President Dennis Sassou Nguesso of the Republic of Congo, during their familiarisation tour of the National Institutes of Health (NIH) in Washington DC July 2, 2014. STATE HOUSE PHOTO.

President Jakaya Mrisho Kikwete enjoys a light moment with President Dennis Sassou Nguesso of the Republic of Congo, during their familiarisation tour of the National Institutes of Health (NIH) in Washington DC July 2, 2014. STATE HOUSE PHOTO.

President Jakaya Mrisho Kikwete speaks with members of the National Institutes of Health (NIH) in Washington DC during a familiarisation tour of the NIH, reputedly the largest hospital and reasearch facility in the world July 2, 2014. STATE HOUSE PHOTO.

President Jakaya Mrisho Kikwete speaks with members of the National Institutes of Health (NIH) in Washington DC during a familiarisation tour of the NIH, reputedly the largest hospital and reasearch facility in the world July 2, 2014. STATE HOUSE PHOTO.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameyataka makampuni na wafanyabiashara wa Marekani kuongeza uwekezaji wao katika Tanzania, akisema kuwa Tanzania inao uwezo wa kupokea zaidi ya mara 10 uwekezaji wa sasa wa makampuni ya Marekani katika Tanzania wa dola za Marekani bilioni 4.5.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa zaidi wa kufanya biashara kubwa zaidi na Marekani kuliko biashara ya sasa kati ya nchi hizo mbili yenye thamani ya dola za Marekani milioni 328.8.
Rais Kikwete ameyasema hayo katika taarifa yake maalum anayoitoa mwishoni mwa wiki hii akikaribisha Mkutano wa Kwanza na wa Kihistoria wa Viongozi wa Marekani na Afrika (USA-Africa Leaders Summit) ulioitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani na unaofanyika kwa siku tatu kuanzia Jumatatu, Agosti 4, 2014 mjini Washington D.C. Nchi 47 za Afrika zimealikwa kushiriki Mkutano huo.
Katika taarifa yake hiyo kwa vyombo vya habari, ambayo pia imetolewa sambamba na Taarifa Rasmi ya Tanzania (Tanzania National Statement) kuhusu mkutano huo, Rais Kikwete amesema:
“Wakati huu wa Mkutano wa Viongozi wa Marekani na Afrika naungana na viongozi wenzangu wa Afrika kumpongeza, kwa namna ya pekee, Mheshimiwa Barack Obama, Rais wa Marekani , kwa kubuni wazo na kuandaa Mkutano huu wa kihistoria wa wakuu wa nchi.”
Ameongeza Rais Kikwete katika kuukaribisha Mkutano huo, “Mkutano huu wa wakuu wa nchi ni ushahidi wa wazi kuthibitisha dhamira ya Rais Obama katika kukuza uhusiano kati ya Afrika na Marekani na pia kuchangia kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Afrika, kwa kufuta umasikini katika Bara letu.”
Rais Kikwete ameongeza na kusisitiza: “Aidha, mkutano huu unatoa nafasi nzuri sana kwa Bara la Afrika kuelezea hadithi yake kuhusu maendeleo ambayo Bara letu linayapata na kupitia katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na kiusalama. Pia Mkutano huo unatoa nafasi nadra sana kwa Bara la Afrika kuwajulisha kwa undani kabisa wafanyabiashara wa Marekani kuhusu fursa za kibiashara na uwekezaji kwenye nchi zetu.”
Akifafanua kuhusu hali ya uwekezaji na uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Marekani, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania iko tayari kufanya biashara na Marekani.
“Kwa hakika, tayari, kuna wawekezaji kadhaa pamoja na wafanyabiashara ambao wanaendesha shughuli zao katika Tanzania. Hata hivyo, tunaamini kuwa uhusiano huu wa uwekezaji na biashara unaweza kuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.”
Rais Kikwete pia ameyataja maeneo ambako makampuni ya Marekani yanaweza kuwekeza, tena kwa haraka, yakiwemo ya utafutaji wa gesi na mafuta, uchimbaji wa madini, kilimo na viwanda vya kilimo, uzalishaji wa viwandani, teknolojia ya habari na mawasiliano na uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Maeneo mengine ambayo Rais Kikwete ameyataja kuwa tayari kwa uwekezaji wa makampuni ya Marekani ni pamoja na ujenzi na uendeshaji wa bandari, ujenzi wa mtandao wa reli na hasa Reli ya Kati na utalii.
Mbali na fursa hizo za uwekezaji, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inazo sifa za ziada kwa ajili ya wawekezaji ikiwa ni pamoja na hali ya amani na utulivu, mazingira rafiki ya kufanyia biashara, jiografia ya Tanzania yenyewe, soko kubwa na linalofikika bila vikwazo kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo kwa pamoja zina soko ya watu kiasi cha milioni 400 na nguvukazi yenye ujuzi.
Rais Kikwete amemalizia taarifa yake kwa kusema: “Mwisho, napenda kusema kuwa Tanzania inayo furaha kubwa sana kuhusishwa na Mkutano huu wa Kihistoria wa Wakuu wa Nchi. Tunayo matarajio makubwa kuhusu matokeo ya Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Marekani na Afrika.”