WHC ni Mkombozi wa Watumishi wa Umma Tanzania

Ofisa Mtendaji Mkuu wa WHC, Dk. Fred Msemwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa WHC, Dk. Fred Msemwa.


Na Mwandishi Wetu, Dar
KWA watumishi wa umma uanzishwaji wa Watumishi Housing Company (WHC) ambao ni mpango wa makazi kwa watumishi wa umma ni mkombozi wa kweli kwa ustawi wa maisha ya mfanyakazi wa serikali, asante kwa serikali ya awamu ya nne kwa kuanzisha taasisi hii muhimu kwa ujenzi wa taifa.
WHC ni taasisi inayojihusisha na uendelezaji miliki na usimamizi wa uwekezaji katika miliki. Kampuni hii ya umma imepewa jukumu la kuwa mtekelezaji mkuu wa mpango wa taifa wa makazi kwa watumishi wa umma na ina jukumu la kujenga nyumba 50,000 nchi nzima.
Akizungumza na mtandao huu mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa WHC, Dk. Fred Msemwa amesema kuwa nyumba hizo zitauzwa kwa mkopo nafuu wa muda mrefu kwa watumishi wa umma.
“Baada ya Benki Kuu kulegeza masharti ya mikopo ya nyumba kwa hiyo sasa mtumishi wa umma haihitaji fedha ya kutanguliza (deposit) ambayo ni tofauti na masharti yaliyopo sasa katika uuzaji wa nyumba kwa mikopo ambayo yanamtaka mnunuzi atoe asilimia 10 mpaka 20 kama fedha ya utangulizi,” anasema Dk. Msemwa
Anasema kwamba WHC ni taasisi ya umma yenye jukumu la uendeleza makazi yaliyo bora kwa watumishi wa umma nchini na ilianzishwa mwaka 2013 na jukumu kubwa ni kuboresha na kujenga makazi ya watumishi wa umma nchi nzima.
Dk. Msemwa alisisitiza kwamba serikali iliamua kuja na utaratibu huo wa makazi kwa watumishi wake baada ya kuona kwamba kwenye nguvu ya soko la makazi watumishi wachache wanaweza kumudu nyumba zinazouzwa na taasisi za fedha kwa sababu ya riba kuwa juu.
Anaongeza kuwa mkopo katika nyumba hizi ni kwa miaka hadi 25 na riba ya nyumba hizi ni asilimia 10 hadi 13 ukilinganisha na hali ilivyo kwenye soko la sasa la nyumba nchini Tanzania.
Dk. Msemwa anasema kwamba ujenzi rasmi wa nyumba hizi za watumishi wa umma zitaanza kujengwa mwezi oktoba mwaka huu sehemu mbalimbali za nchi kama vile Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Arusha, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Dodoma, Morogoro, Mbeya, Lindi na Mtwara.
Anaeleza kuwa inakadiriwa kwamba kuna wafanyakazi 650,000 wanaofanya kazi kwenye mashirika na sekta ya umma ambapo wafanyakazi 10,000 sawa sawa na asilimia 2 tu tu waliopata mikopo ya nyumba.
Aliongeza; WHC wameweza kufika hapo walipo baada ya kupata Baraka ya kuwa chini ya mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo ni Mfuko wa PPF, National Social Security Fund (NSSF), Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa Umma (PSPF), LAPF, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali (GEPF), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Pia kampuni hiyo ina jukumu la kusimamia vipande vya uwekezaji katika miliki (Real Estate Investment Trusts –REITs).
“kila mtumishi wa umma atanunua nyumba kwa kupitia mkopo kwa kuangalia kiwango chake cha mshahara kama mtumishi wa umma,” alisisitiza
Dk. Msemwa alifafanua kwamba tofauti kati ya WHC ni mabenki na kampuni zingine ni kwamba wengine wanafanya biashara kwa kuangalia faida ila taasisi wana malengo ya kuhakikisha mtumishi wa serikali anapata makazi bora ya kuishi kabla na baada ya kustaafu.
Anasema kwamba kuanzia katika Mkoa wa Dar es Salaam nyumba zitajengwa Mabwepande, Magomeni na Kigamboni baada ya kukamilisha taratibu zote kwa kushirikiana na serikali za mitaa na wizara ya ardhi na maendeleo ya makazi ili kuhakikisha maeneo yote yanakuwa na hati miliki (title deeds).
Dira ya WHC ni “Makazi Bora kwa Watumishi wa Umma” na Dhima kuwezesha watumishi wa umma kumiliki nyumba kwa njia ya mikopo nafuu na kufaidi matunda ya uwekezaji katika miliki kwa kutumia wafanyakazi wenye weledi katika usimamizi wa uwekezaji na uendelezaji miliki.