WAKAZI wa Kijiji cha Masusu, Kata ya Gisambalang wilayani Hanang’ katika Mkoa wa Manyara wamepatwa na mshtuko kutokana na tukio lenye utata la kuuawa mtoto Omary Hamis mwenye umri wa mitatu, kisha mwili wake kutundikwa juu ya mti. Inadaiwa kuwa Omary aliuawa na watoto wenzake wawili ambao ni wakazi wa kijiji hicho kwa kumpiga kwa fimbo kisha kumnyonga na baadaye kuutundika mwili wake juu ya mti.
Watoto wanaodaiwa kufanya kitendo hicho (majina yao tunayahifadhi kwa sasa), mmoja ana umri wa miaka mitano na mwingine miaka saba na wote wanashikiliwa na polisi katika Kituo cha Katesh, mkoani Manyara kwa uchunguzi zaidi.
Diwani wa Kata ya Gisambalang, Masala Bajuta alisema tukio hilo lilitokea Julai 26, mwaka huu saa 7 mchana na kwamba watoto wanaodaiwa kufanya kitendo hicho walikuwa wakichunga mifugo ndipo walipokutana na mtoto mwenzao.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili kutoka kijijini Masusu zinasema Omary ambaye ni mkazi wa Babati, alikuwa amepelekwa kwa babu yake anayeishi kijijini hapo kwa ajili ya kumsalimia, hivyo alikuwa mgeni katika eneo hilo.
Akiwa anacheza katika eneo linalozunguka nyumba ya babu yake, Omary alitoweka na hakuonekana tena hadi pale taarifa za mwili wake kukutwa umetundikwa kwenye mti zilipoifikia familia yake ambayo wakati huo ilikuwa ikimtafuta.
Bajuta alisema siku ya tukio hilo Omary alipotea njia na kukutana na watoto wenzake wawili waliokuwa wakichunga ng’ombe na kuanza kumwongelesha Lugha ya Kidatoga ambayo haielewi kwa kuwa yeye ni Mburunge kutoka Wilaya ya Babati.
“Baada ya kumuuliza jina lake kwa lugha yao na yeye akawa haijui na kushindwa kujibu, watoto hao walianza kumpiga kwa fimbo, wakamnyonga na kisha wakamtundika juu ya mti,” alisema Bajuta.
Alisema ndugu wa Omary walianza kumtafuta mtoto huyo baada ya kutoonekana, na baada ya muda mama yake mkubwa alimuona akiwa ametundikwa kwenye mti akiwa ameshafariki dunia. Taarifa za ushiriki wa watoto hao katika tukio la kuuawa Omary, zilitolewa na mtoto mwingine ambaye alishuhudia tukio hilo. Mtoto huyo muda wote wakati marehemu akitafutwa, alikuwa kimya lakini baadaye aliwaambia wazazi wake kwamba Omary ‘amekaa juu ya mti’.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki alisema watoto hao wawili wanashikiliwa na polisi wakidaiwa kumuua mtoto huyo.
“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili, kwani ni jambo ambalo limetushangaza kutokana na mazingira ya kifo chenyewe na umri wa watoto hao wawili wanaodaiwa kufanya mauaji hayo,” alisema Kamanda Nsimeki.
Nsimeki alisema wamehifadhiwa katika mahabusu ya watoto katika Kituo cha Kateshi.
CHANZO: Mwananchi