WAZIRI wa Habari nchini Liberia, Lewis Brown ameomba msaada nchi yake kusaidiwa kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola unaolikabili taifa hilo. Amesema Liberia inahitaji msaada toka Jumuiya za Kimataifa ikiwa ni pamoja na kutumiwa wataalam wa tiba ili wasaidie kidhibiti ugonjwa huo.
Waziri huyo ameuelezea mlipuko wa ugonjwa huo kuwa si wa kawaida hivyo wanaomba kusaidiwa. “Huu bado ni mshituko. Uwezo wa huduma za afya ya jamii na vifaa vimezidiwa. Maambukizi na kutapakaa ni kwa namna ambayo hatukuwahi kuwa nayo. Tunapungukiwa wahudumu wa afya na kwakweli tunahitaji wataalam zaidi wa afya,” alisema Brown.
Alisema Liberia inahitaji vifaa vya huduma za kiafya, wataalam wenye uzoefu wa kiafya kutokana na hali ya ugonjwa huo ulivyo; “tunahitaji chochote kinachoweza kutusaidia kupambana na ugonjwa wa Ebola,” amesisitiza.
Serikali ya Uingereza imeitisha mkutano wa dharura kupanga hatua za kuchukuliwa kwa ushirikiano na serikali ya Ufaransa na Marekani. Umoja wa Ulaya imetenga dola milioni 2 nukta 5 za ziada ili kupambana na Ebola. Tangu Ebola ilipoanza mwezi Februari, 2014, zaidi ya watu 670 wamefariki huko Afrika Magharibi katika nchi za Sierra Leone, Liberia, Guinea na Nigeria.
-BBC