JK Aleta Neema kwa Wakulima wa Mpunga na Matunda

mpunga ukiwa tayari kuvunwa

mpunga ukiwa tayari kuvunwa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Jumatatu, Julai 28, 2014, amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Atomiki na Nishati (IAEA) Yakuya Amano.
Katika mazungumzo yao Ikulu, Dar Es Salaam, viongozi hao wawili wamebadilisha mawazo ya jinsi IAEA linavyoweza kuisaidia Tanzania kuongeza uzalishaji wa mbegu mpya ya mpunga ambayo utafiti wake ulifanyika Tanzania Visiwani na kuendeshwa na Shirika hilo.
Aidha, Rais Kikwete na mgeni wake wamezungumzia jinsi Shirika hilo linavyoweza kusaidia Tanzania kupata utaalam wa kutunza matunda na mboga kwa muda mrefu zaidi bila kuharibika ama kuoza kwa kutumia utalaamu wa mionzi.
Amano, raia wa Japan ambaye amekuwa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA tokea Desemba mosi mwaka 2009, amemwambia Rais Kikwete kuwa baada ya kutembelea Tanzania huko nyuma ameipenda nchi kiasi cha kuamua zamu hii kuja kutembelea kwa mapumziko.
Amano ni Mkurugenzi Mkuu wa tano tokea kuanzishwa kwa Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Vienna, Austria, mwaka 1957.
Rais Kikwete kwa upande wake amemshukuru Amano kwa misaada ambayo Shirika lake limekuwa linatoa kwa taasisi za Tanzania ikiwamo Hospitali ya Ocean Road na Shirika la Uthibiti wa Dawa na Chakula (TDFA).