TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA WATANZANIA WOTE
Ndugu Wanahabari
Hivi karibuni viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyakazi pamoja na mamlaka ya kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii (SSRA), Wametoa matamko yanayokinzana juu ya mifuko ya jamii kwa wafanyakazi.
Ndugu wanahabari
Taarifa hiyo yenye kukinzania iliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari, likiwamo gazeti la Nipashe la Julai 24, 2014 ukurasa wa kwanza na watano, ambapo Nicholas Mgaya, Katibu Mkuu wa TUCTA; Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania alikaririwa akisema wamepeleka mapendekezo serikalini juu ya kutaka mifuko mingine iwe karibia au sawa na LAPF au PSPF. Wakati Mgaya anasema hivi, Gratian Mkoba Rais wa CWT; Chama cha Walimu Tanzania na Boniface Nkakatisi, Katibu Mkuu wa TUICO, alinukuliwa akisema Serikali na SSRA wanamapendekezo juu ya kupunguza 30% kutoka 50% ya mafao kwa LAPF na PSPF.
Ndugu wanahabari
SSRA, kwa upande wao wanakana kuwepo kwa waraka wowote juu ya hilo, huku wizara yenye dhamana na hili (wizara ya kazi na Ajira) imekaa kimya. Kwa mujibu wa sheria na taratibu za kusimamia maslahi ya wafanyakazi, hawa wanao kinzana ni watu waliopaswa kuwa na majibu sahihi juu ya hili. Kwani hadi sasa wafanyakazi hawana majibu yanayoeleweka.
Ndugu wanahabari
Kwa mujibu ya sheria ya usimamizi wa mifuko ya jamii sheria namba 8 ya mwaka 2008, kifungu cha 25 (1) SSRA ndiyo wana mamlaka ya kutoa viwango vya ulipaji wa mafao na kusimamia viwango hivyo pamoja na Serikali. Kama wao wakiwa hawajui na Serikali ikikaa kimya wafanyakazi wakimbilie wapi?. Wafanyakazi wanahitaji Taarifa sahihi juu ya mafao yao.
Ndugu wanahabari
Nimekuwa nikipokea simu na jumbe nyingi kutoka kwa wafanyakazi wakiomba kutolewe tamko linaloeleweka ili wajue ukweli ulivyo. Ifahamike kuwa kupigania haki na maslahi thabiti ya wafanyakazi bila woga ni kipaumbele change namba moja kama Rais mtarajiwa wa TUCTA.
Ndugu wanahabari
Nitoe rai kwa waajiri wote Tanzania, watoe mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao, hii ni kwa mujibu Sheria ya ajira na mahusiano kazini namba 6 ya Mwaka 2004, hasa makampuni ya kigeni, ya wazawa na hata Serikali, waajiri timizeni wajibu wetu tafadhali.
Ndugu wanahabari
Tunatoa tamko na kulaani vitendo vya waajiri kutowatendea haki wafanyakazi wao kwa kutowasajili kwenye mifuko ya jamii au kutofikisha makato yao. Hii ni kinyume cha kifungu cha 30 Sheria ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii, kinaeleza kwa kiingereza
“Every employer in the formal sector shall be required to register his employees with any of the mandatory schemes, provided that it shall be the right of the employee to choose a mandatory scheme under which the employee shall be registered”
Tafsiri japo sio ya moja kwa moja “kila muajiri kwenye sekta iliyo rasmi ni lazima awasajili waajiriwa kwenye mifuko ya jamii, na ni haki ya muajiriwa kuchagua mfuko anaoutaka”. Ni kinyume cha haki za binadamu kumnyima mtu fursa ya kupata haki ya mifuko ya hifadhi ya jamii. Mkataba wa kimataifa wa uchumi,jamii na Tamaduni wa mwaka 1966 (Interanational Covenant on Economic Social and Cultural Right) Fungu la 9 inasema nchi wanachama (ikiwamo Tanzania) kutoa haki ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wake, Tunatoa wito wa dhati kuzitiwa hili.
Ndugu wanahabari kuna hoja kuhusu walioajiriwa Uhamiaji
Kumekuwa na mijadala inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo kupitia mitandao ya kijamii kwamba kuna watu ambao ni aidha ndugu ama jamaa wa wafanyakazi wa Uhamiaji waliopewa fursa ya kuajiriwa zaidi Uhamiaji baada ya usaili wa kihistoria wa hivi karibuni uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam uliohusisha watu zaidi ya 10,000 kufanyiwa usaili kwa ajili ya kujaza nafasi 70.
Tunaomba Uhamiaji kujibu tuhuma hizi ili wananchi wote tufahamu ukweli. Katika baadhi ya mitandao ya kijamii yametajwa hadi majina ya walioajiriwa na ndugu au jamaa zao Uhamiaji. Katika hali kama hii, haitakuwa sahihi kwa Uhamiaji kukaa kimya. Ni vema tamko rasmi likatolewa ili wananchi wa Watanzania Tanzania tukafahamu ukweli hasa ukoje.
Ndugu wanahabari na Watanzania kwa ujumla tunawatakia sikukuu njema; kila Mtanzania aliyeajiri mtu mmoja na kuendelea ajitafakari vizuri kama anachomfanyia huyo mtu au hao watu ni sahihi; kwa kufanya hivi tutakuwa watenda haki wazuri kwa wafanyakazi.
Imetolewa leo Julai 28, 2014
na Dismas Lyassa Imesainiwa kwa niaba ya Mgombea na
(Mgombea Uraisi TUCTA)
0754 49 8972/0712183282
Wakili Jebra Kambole
(Wakili wa Dismas Lyassa; Mgombea Uraisi TUCTA)
+255 717 334032
NB: -Uchaguzi wa Uraisi wa TUCTA utafanyika tarehe 4-5, 2014, Dodoma.
-Jebra Kambole ni wakili kutoka Kampuni ya Uwakili ya Law Guards ya Jijini Dar es Salaam
*Nakala:
Uhamiaji Makao Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Spika, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani na Kituo cha sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa ufuatiliaji