Na Anna Nkinda – Maelezo, Nachingwea
WANAFUNZI wa kike wa vyuo vya ualimu nchini wametakiwa kuvaa mavazi nadhifu yanayoendana na maadili ya kazi yao ili wanafunzi na jamii inayowazunguka ijifunze kutoka kwao kwani wao ni kioo cha jamii.
Mwito huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na baadhi ya wanafunzi wa kike wa chuo cha Ualimu Nachingwea mara baada ya kumalizika kwa futari aliyoiandaa kwa ajili ya viongozi wa wilaya iliyofanyika chuoni hapo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema siyo jambo jema kwa mwalimu kuvaa mavazi yanayoonyesha sehemu za miili yao ikiwemo kata mikono, nguo zinazobana na sketi fupi kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na haiba ya ualimu.
“Sikuhizi kuna baadhi ya watu wanavaa mavazi yasiyoendana na utamaduni wa mtanzania, nyinyi kama walimu ambao ni kioo cha jamii na mnawafundisha wanafunzi madarasani msifanye hivyo kwa kufanya hivyo watoto wataiga na kufikiria kuwa kuvaa mavazi hayo ni sawa,” alisema.
Mama Kikwete pia aliwataka wanafunzi hao kutokuchagua maeneo ya kwenda kufanya kazi pindi wamalizapo masomo yao na kupangiwa vituo vipya vya kazi kwani kazi ya ualimu ni wito na kama mtu hakuipenda kazi hiyo basi angechagua fani nyingine za kusoma.
“Baadhi ya walimu wamekuwa wakikataa kwenda kufanya kazi katika maeneo ya vijijini, na wengine wakipangiwa vituo vya mbali na mjini wanaogopa na kudiriki hata kuacha kazi, kama ni hivyo kwa nini ulipoteza fedha na muda wako kusomea ualimu?”, aliuliza Mama Kikwete.
MNEC huyo alimalizia kwa kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi wawapo masomoni kitendo ambacho kitawasaidia kumaliza masomo yao salama na kurudi nyumbani bila ya kufukuzwa chuo kwa ajili ya kupata ujauzito.
Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni mwalimu miaka ya nyuma alisoma chuo cha ualimu Nachingwea na juzi akiwa chuoni hapo alitembelea Bweni la wasichana la Kawawa ambalo ndilo alilokuwa analala wakati akiwa mwanafunzi wa chuo hicho.