Na Mwandishi wa Jeshi la Polis- Pemba
BALOZI wa Polisi Jamii nchini, Bi. Rahma Al-Kharoosi ametoa sh. milioni 10 fedha ambazo zitatumika kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya katika kituo cha kuhifadhia vijana walioathiriwa na dawa hizo.
Sambamba na hayo, Ofisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, amewataka wananchi kuendelea kuwafichua wale wote waliopo kwenye mtandao wa kujihusisha na uingizaji, usambazaji na hata uuzaji wa dawa za kulevya ili wakamatwe.
Wito huo umetolewa leo mjini hapa na wakati Bi. Rahma na ujumbe kutoka Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulipokuwa ukitembelea waathirika wa dawa za kulevya Kisiwani Pemba.
Akizungumza na kundi la vijana wa kituo hicho, waliopo chini ya uangalizi maalumu wa kituo, Bi. Rahma amesema kuwa wakati umefika wa kuwataja wale wote wanaojihusisha na kusambaza dawa hizo kwa jamii.
Hata hivyo ameongeza kuwa kama kila kijana aliyeathirika ataamua kumtaja aliyesababisha yeye kuathirika ni wazi kwamba Jeshi la Polisi litawafuatilia na kuwakamata, hivyo kupunguza tatizo la ongezeko la dawa hizo hapa nchini.
Bi. Rahma amesema hakuna haja ya kuendelea na dhana ya kwamba; mtu anapomtaja mmoja au kundi la watu waliopo kwenye mtandao huo wa watu wanaojihusisha na uagizaji, uingizaji, usambazaji na uuzaji wa dawa hizo kuwa atauawa.
Amesema dhana hiyo ni potofu na imekuwa ikiwapa kiburi wafanyabiashara hao pamoja na washirika wao, kwani inawafanya waonekane wana nguvu kubwa zaidi ya polisi na Serikali nzima.
Amesema kuwa kwa vile wanaoathirika zaidi na dawa hizo ni vijana na wengi wao wakiwemo watoto kutoka familia masikini ambazo zimekuwa zikitegemea kupata mahitaji muhimu ya kujikimu na sasa wanakosa huduma hizo, hakuna haja ya kuendelea kuwaficha watu hao ambao ni sawa na wauaji.
Bi. Rahma amesema kuendelea kuwafichia siri watu hao kwa kuhofia usalama wa watoa taarifa, ni kuendeleza tatizo la ongezeko la dawa hizo na hivyo kuongeza pia ongezeko la vijana tegemezi katika familia duni.
Balozi huyo wa Polisi Jamii nchini, amempongeza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamadi, kwa juhudi za kukabiliana na tatizo la mihadarati ikiwemo ya kutoka viwandani na hata mashambani.
Bi. Rahma, ametaka Juhudi hizo ziungwe mkono na kila mmoja wakiwemo viongozi wengine wa Serikali na vyama vya siasa ili kwa pamoja waweze kulikomboa taifa katika dimbwi la dawa za kulevya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Bi Mwanajuma Magid Abdul, na Mwakilishi wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bw. Juma Bakari Alawa, wamesema tayari Serikali imeweka mikakati ya kupunguza ongezeko la dawa za kulevya visiwani humo.
Amesema kupitia Jeshi la Polisi, mikakati ya kuwapeleleza na kuwabaini wale wote wanaojihusiosha na biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini imewekwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, ACP-Hassan Nassir na Mkuu wa Polisi wilaya ya Mjini Unguja, SSP-Mkadam Khamis Mkadam, wameomba wananchi na wafanyabiasha kujitokeza kusaidia taasisi zinazowahudumia vijana walioathirika na dawa hizo kwani hilo ni sawa na janga la kitaifa.