Na Joachim Mushi
MTANDAO wa Wanawake na Katiba nchini Tanzania umewakutanisha baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba pamoja na Wajumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba kujadili namna ya kushinikiza masuala ya haki za wanawake kuingizwa katika rasimu ya pili ya Katiba Mpya.
Semina hiyo iliyoshirikisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari pamoja na wanahabari imeanza leo katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam na itafanyika kwa siku mbili yaani Julai 24 na 25, 2014.
Akizungumza kukaribisha washiriki wa mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka alisema wajumbe katika mkutano huo watajadili umuhimu wa kuimarisha masuala ya haki za wanawake katika Katiba.
Alisema kuwa wajumbe pia watajadili namna ya kutetea na kulinda masuala muhimu ya haki za wanawake yaliyojitokeza katika rasimu ya pili ya Katiba Mpya ikiwa ni pamoja na kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusiana na masuala ya katiba yenye maslahi ya wanawake na taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), Mary Rusimbi ambao ni moja ya taasisi zilizoratibu mkutano huo, alisema pamoja na mambo mengine madhumuni ya mkutano huo ni kuwawezesha wabunge wanawake kwa wanaume katika Bunge Maalum la Katiba na wanaharakati wa jinsia na haki za wanawake kuimarisha hoja zao.
Katika mkutano huo wahariri wa vyombo anuai vya habari kwa nyakati tofauti waliwataka wajumbe hao kuvitumia ipasavyo vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano ili hoja zao ziingie katika vyombo hivyo na kuifikia jamii.
Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa bunge maalum la Katiba wakizungumza kujibu baadhi ya maswali ya wahariri wa habari walisema wamejipanga kupaza sauti kuhakikisha hoja zao wanazozipigania zinaingizwa katika Katiba Mpya.
Naye Mjumbe wa Bunge Maalum, Dk. Avemaria Semakafu alivitaka vyombo vya habari kuendelea kuwaunga mkono wanamtandao hao ili kupigania kero za akinamama na wananchi kwa ujumla na kuhakikisha zinapata majibu katika mchakato wa uundaji katiba mpya.