Nyumba za Taasisi ya Mkapa Zazinduliwa Tunduru

Mwanzilishi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa.

Mwanzilishi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Julai 22, 2014, amezindua mradi wa nyumba 40 za watumishi wa sekta ya Afya katika Mkoa wa Ruvuma ambazo zimejengwa na Taasisi ya Benjamin W. Mkapa katika sherehe iliyofanyika Matemanga, Wilaya ya Tunduru, Ruvuma. Nyumba hizo ni sehemu ya nyumba 480 zinazojengwa na Taasisi hiyo ya Rais wa Tatu wa Tanzania katika Halmashauri 48 za Mikoa 16 nchini chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Huduma za Afya unaogharimiwa na Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria – Global Fund.

Nyumba hizo zinajengwa katika mikoa ya Mtwara (nyumba 50), Rukwa (40), Singida (30), Ruvuma (40), Lindi (60), Morogoro (20), Pwani (20), Arusha (20), Mwanza (20), Kigoma (30), Geita (20), Manyara (30), Kagera (20), Simiyu (50), Shinyanga (40) na Tanga (10).

Mpaka sasa Taasisi ya Benjamin W. Mkapa imekamilisha ujenzi na kukabidhi nyumba 140 zilizoko Mtwara, Rukwa, Singida na Ruvuma. Nyumba hizo za kisasa kabisa zinajengwa na Taasisi ya Benjamin W. Mkapa chini ya makubaliano ya miaka mitano ambayo mwaka 2011, Taasisi hiyo ilifikia na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako Taasisi hiyo inatekeleza Mradi huo mkubwa ambao unalenga kupunguza uhaba wa nyumba za watumishi wa afya nchini.

Katika eneo hilo la Matemanga, Rais Kikwete amezindua nyumba mbili kati ya 40 zinazojengwa katika mkoa wa Ruvuma katika Halmashauri za Wilaya za Mbinga, Namtumbo, Songea Vijijini na Tunduru ambako kila Halmashauri inajengewa nyumba 10. Nyumba hizo zinajengwa katika vituo 20 vya tiba, iwe kwenye zahanati ama vituo vya afya, ambako kila kituo kinajengewa nyumba mbili kikiwemo cha Matemanga.

Nyumba hizo zinajengwa katika Halmashauri, Wilaya na Mikoa yenye uhababa mkubwa zaidi wa nyumba za watumishi wa sekta ya Afya kama Mkoa wa Ruvuma ambao mwaka juzi ulikuwa na vituo 129 vya tiba lakini ina nyumba 22 tu za watumishi wa vituo hivyo.

Mkoa huo ulikuwa na uhaba wa nyumba 107 na hivyo kuwa na uhaba wa asilimia 82, na kwa kupata nyumba 40 mpya, uhaba huo umepungua kwa kiasi cha asilimia 37.

Ujenzi wa nyumba hizo 40 umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.7 ikiwa ni wastani wa shilingi milioni 67 kwa kila nyumba. Nyumba 38 kati ya hizo ni za aina ya vijijini ambazo zinatumia umeme wa jua na mbili ni aina ya nyumba za mjini ambazo zinatumia umeme wa gridi ya taifa.

Kila nyumba kati ya nyumba hizo ina sebule, veranda, baraza, eneo la jiko, nyumba vitatu vya kulala, uzio wa tofali, tenki la maji lita 500, mfumo wa kuvuna maji ya mvua na mfumo wa umeme wa nguvu za jua ama wa gridi.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Kikwete ametoa pongezi maalum kwa Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba hizo na akatoa shukurani maalum kwa Mzee Mkapa kukubali kuendelea kuwatumia Watanzania hata katika wakati wake wa kustaafu.

“Angeamua kwenda kutulia kwao Lupaso, lakini kwa mapenzi ya utumishi wa wananchi wenzake, amekubali kuendelea kuwatumikia kupitia njia hii ya sekta ya afya,” amesema Rais Kikwete.

Aidha, Rais Kikwete ametoa shukurani maalum kwa Global Fund kwa kuendelea kuisaidia Tanzania na Watanzania kupambana na Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria na kuongeza kuwa misaada yao imeokoa maisha ya mamilioni ya Watanzania na kuleta tofauti kubwa katika maisha yao.