WAKATI Serikali ya Japan ikikanusha kuwa samaki waliosafirishwa kuja nchini hawana aina yoyote ya mionzi hatari kwa binadamu, Tanzania imesema wizara tatu zinatarajia kukutana hivi karibuni ili kutoa tamko rasmi kuhusu samaki hao.Jumla ya tani 125 za samaki hao wanadaiwa kuwa na mionzi ya nyuklia ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Ubalozi wa Japan nchini, jana ulitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa Shirika la Uvuvi la Japan chini ya Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi ya Japan, liliwasiliana na Kampuni ya Kaneyama Corporation, ambayo ndiyo ilisafirisha hao samaki kuja Tanzania na walithibitisha kwa nyaraka kutoka Shirika la Japan Frozen Inspection Corporation kwamba tani 124.992 za samaki waliosafirishwa kuja nchini Tanzania hazina aina yoyote ya mionzi
hatari kwa binadamu.
Mbali na hilo taarifa hiyo ya ubalozi ilieleza kwamba samaki hao walivuliwa katika mwambao wa Choshi, Chiba Prefecture Desemba 16-17, mwaka jana na kusafirishwa hadi Bandari ya Hasaki iliyopo Ibaraki
Prefecture Desemba 17 mwaka 2010.
“Kwa msingi huo samaki hawakuathirika na mionzi ya nyuklia. Tunapenda kuhitimisha kuwa hawa samaki wa mackerel kutoka Japan wamezoeleka hapa nchini Tanzania kutokana na urahisi wa kupatikana pamoja na matumizi mazuri. Pia wamekuwa chanzo cha protini kwa walaji, hivyo ni imani yetu kuwa ulaji wa samaki hawa utaendelea,”.
Lakini kwa upande wa Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni alisema jana kwamba ripoti za wataalamu tayari zimekamilika na kinachosubiriwa ni wizara tatu kuzijadili na kutoa kauli ya Serikali.
“Tunatarajia kukutana wizara tatu… Tamko litakalotolewa ndilo litakuwa msimamo wa Serikali,” alisema Nyoni akisema kikao hicho kitafanyika wakati wowote baada ya kukamilisha mawasiliano ya wizara zote na kukubaliana siku maalumu.
Katibu huyo alizitaja wizara hizo kuwa ni wizara yake, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.Nyoni alisema wananchi wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhari ya kutonunua samaki hao.
Tamko la Nyoni limekuja huku kukiwa na taarifa kwamba Tume ya Mionzi Tanzania (TAEC) ya mjini Arusha kupitia ripoti yake iliyokabidhiwa serikalini wiki iliyopita, inaeleza kwamba haikubaini kuwepo kwa mionzi hatari.
Nyoni alikataa kuzungumzia lolote juu ya ripoti hiyo ya TAEC akisema itatolewa baada ya wizara tatu zitakapojiridha kutokana.Akitoa taarifa ya Serikali za hivi karibuni, Nyoni aliutahadharisha uma kuwa athari za sumu inayohofiwa kuwamo kwenye samaki hao athari zake siyo za ghafla bali huenda polepole.
Alisema Serikali ilizuia usambazaji wa samaki hao wakati ambapo kilo nyingi tayari zilikuwa zimesambazwa katuka Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro.Lakini akasema Serikali na taasisi mbalimbali za umma zipo kwenye msako wa usiku na mchana ili kufanikisha suala la kuwakamata na kuwarejeshi samaki waliosambazwa kwenye masoko mbalimbali.
“Wananchi wanaombwa kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Idara za Afya za Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro na Jeshi la Polisi, ili samaki waliobaki wapatikane na kurejeshwa ofisi za mamlaka za afya na Jeshi la Polisi zilizo jirani au Kampuni ya Alphakrust Ltd,” alionya Nyoni.
Alifafanua, “Samaki wenye uzito wa tani 1.319 wanafuatiliwa na kumbukumbu kutoka kampuni hiyo zinaonyesha kuwa wamesambazwa kupitia soko la Feri, Dar es Salaam, Morogoro Mjini na Kilombero.”Katika kuhaha ili kuokoa maisha ya Watanzania, Nyoni anasema: “Wizara inaviomba vyombo vya habari, viiarifu na kuielimisha jamii juu ya kuwapo kwa samaki wanaochunguzwa kwa kuhisiwa kuwa na madhara.”
Pamoja na juhudi hizo, alifafanua “kazi hii ya ufuatiliaji na uchunguzi inaendelea usiku na mchana hadi samaki hao watakapopatikana.”
Nyoni alisema samaki hao aina ya “Mackerel” waliingizwa nchini na kampuni ya Alphakrust Ltd ya Dar es Salaam kutoka Kampuni ya Kaneyama Corporation ya Chiba, Japan.
“Samaki hao walisafirishwa kupitia Bandari ya Yokohama, Japan na kuingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Nyoni akidai kuwa taarifa zinaonyesha waliingizwa baada ya kukidhi masharti ya kisheria na taratibu zilizowekwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa.
“Kwa mujibu wa nyaraka za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mzigo huo ulifika Bandari ya Dar es Salaam Julai 18 mwaka huu,” alisema Nyoni, akifafanua:
“Wizara ilipata taarifa siku ya Jumamosi kwamba samaki hao wanahisiwa kuchafuliwa na mionzi ya nyuklia iliyotokea huko Japan, Machi mwaka huu”.Kulingana na uchunguzi uliofanywa na wizara yake, alisema Samaki hao walisindikwa tangu Desemba mwaka jana 2010 na muda wake wa mwisho wa kumbukumbu unaonyesha muda wake wa mwisho wa matumizi ni Juni, 2012.
CHANZO: Mwananchi