Dodoma,
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imeshusha bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kunzia leo. Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Chuo cha VETA mjini hapa, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu alisema bei ya petroli imeshuka kwa Sh202.37 kwa lita ambayo ni sawa na asilimia 9.17. Dizeli imeshuka kwa Sh173.49 ambayo ni sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa yameshuka bei kwa 181.37 sawa na asilimia 8.70.
Masebu alisema kutokana na viwango hivyo vipya, bei ya kikomo ya petroli katika jiji la Dar es Salaam itakuwa Sh2,004 kwa lita moja, dizeli Sh1,911 na mafuta ya taa Sh1,905. Jijini Arusha bei ya kikomo itakuwa 2,088 kwa petroli, Sh1,989 kwa mafuta ya taa na Sh1,995 kwa dizeli. Dodoma mjini bei itakuwa Sh2,062 kwa lita moja ya petroli, mafuta ya taa 1,963 na dizeli 1,960.
Alisema kushuka kwa bei hizo kumetokana na kukamilika kwa mchakato wa kuandaa kanuni mpya ya ukokotoaji wa bei za bidhaa za mafuta hasa kutokana na maagizo ya Serikali na pia kubadilika kwa viwango vya kodi katika bidhaa za mafuta.
“Kwa ujumla tozo hizi ni asilimia 2.6 na ilipendekezwa zipunguzwe kwa asilimia 50 lakini sisi baada ya kukokotoa tumepunguza kwa asilimia 51.44,” alisema Masebu.
Hata hivyo, alisema kupanda kwa bei ya mafuta kwa kiasi kikubwa, hakutokani na tozo hizo, bali kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na pia kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Alisema baada ya kuanza kwa mchakato wa kupitia mabadiliko ya tozo, petroli imeshuka kutoka Sh54 hadi Sh27 kwa lita, mafuta ya taa kutoka Sh54 hadi Sh28 kwa lita na dizeli kutoka Sh55 hadi Sh24 kwa lita.
“Bei hizi zimepungua kwa nchi nzima kuanzia leo na kituo kitakachokutwa kimepandisha bei tofauti na ile ya kikomo faini yake ni Sh3 milioni kwa kila shilingi moja ambayo itakuwa imeongezwa,”alisema Masebu.
Aliwataka watu wanaopata huduma za mafuta kuhakikisha wanapewa risiti katika vituo ili iwe rahisi kuwabana wamiliki wa vituo wenye bei za juu na ambao watabainika.
Kushuka kwa bei hizo kumekuja baada ya serikali kupokea malalamiko mengi ya wananchi kuhusiana na bei za mafuta kuendelea kupanda tofauti na nchi jirani.
CHANZO: Mwananchi