CCM Kuwachunguza Lowassa, Sumaye, Membe na Wassira

Pichani ni Edward Lowassa, Fredrick Sumaye, Benard Membe na January Makamba.

Pichani ni Edward Lowassa, Fredrick Sumaye, Benard Membe na January Makamba.

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kufanya tathmini kwa wanachama wake ambao iliwaadhibu kwa kile kuonesha utovu wa nidhamu kwa wao kuanza kampeni za kugombea urais ndani ya chama hicho mapema kabla ya muda kutangazwa.

Mapema Februari 2014, CCM iliwaadhibu waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, mawaziri Benard Membe, Stephen Wassira na Naibu Waziri, January Makamba pamoja na aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja kwa kile kuonekana kuanza kampeni mapema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam, kufuatia kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika jijini Dar es salaam, kilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia tena ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya Kamati Kuu kutafakari imeshauri baadhi ya wanachama wake kuzingatia Katiba, Kanuni na taratibu za Chama hicho zinazosimamia masuala hayo ili wasijikute wanapoteza nafasi ya kugombea nafasi wanazohitaji kwa kuadhibiwa.

“…Kuhusu wale waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za Chama kwa suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio ya mwenendo wao wa utekelezaji wa adhabu hiyo mwezi wa nane (Agosti 2014), na kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekeza kwa Kamati Kuu kuongezwa kwa adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji wa masharti ya adhabu husika,” ilisema taarifa hiyo ya CCM.

Taarifa hiyo imesema kuna kila sababu ya wanachama wote wa CCM wakakumbuka kuwa Chama ni pamoja na Katiba, Kanuni na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga, jambo ambalo halivumiliki ndani ya chama hicho.

“…Nia ya CCM kusimamia haya ni kuhakikisha Chama kinakuwa na umoja na mshikamano ambao ni muhimu sana, hasa tunapoelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,” ilisema taarifa hiyo ya CCM.

Julai 16, 2014 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ilifanya kikao cha kawaida cha siku moja mjini Dar es salaam. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimepokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa upande wa pili.

Mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi yana lengo la kuangalia kwa kina ni kwa nini baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalum la Katiba walisusia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo, na kuangalia namna watakavyorudi ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini.

“…Kwa ujumla Kamati Kuu ya CCM imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo na kupongeza juhudi hizo zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa na Vyama husika. Kamati Kuu inapenda kueleza imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda kwa wajumbe wachache waliosusia Bunge Maalum la Katiba, kurejea Bungeni na kumalizia sehemu ya mchakato uliobakia. Kamati Kuu inayatakia kila la kheri mazungumzo hayo.”