Yohane Gervas, Rombo
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), imedhamiria kupunguza umasikini katika familia kupitia mpango wa kunusuru hali ya umasikini kwenye kaya unaotekelezwa na mfuko huo katika awamu ya tatu. Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa uwezeshaji wa Mafunzo TASAF, Fariji Michael, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Ladislaus Mwamanga, kwenye ufunguzi wa warsha ya siku tano ya kuwajengea uwezo na uelewa wadau wake kuhusu mpango wa awamu ya tatu wa kunusuru hali ya umasikini hafla iliyofanyika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Alisema walengwa wa mpango huo uliozinduliwa Agosti 2012 na Rais Jakaya Kikwete, ni kaya zinazoishi mazingira hatarishi na kukabiliwa na umasikini mkubwa. Alisema watakaonufaika na mpango huo ni watoto chini ya umri wa miaka mitano, wanafunzi wa shule za awali na shule za msingi pamoja na kutoa ruzuku kwenye kaya zenye wananfunzi wanaosoma katika shule za sekondari.
Alisema mpango huo pia unajumuisha pogramu za uwasilishaji miradi ya ujenzi, kuimarisha uwezo wa kujikimu na kuendeleza miundombinu inayolenga sekta za elimu, afya pamoja na maji.
Aidha Michael aliongeza kuwa katika mpango huo wakunusuru kaya masikini watatoa ruzuku kwa kaya masikini na ajira kwa wenye uwezo wa kufanya kazi kwenye kaya husika, ambapo watapata ujira utakaowasaidia kuinua hali yao ya kimaisha.
Awali akifungua warsha hiyo Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Elinas Pallangyo mbali na kushukuru mpango huo kufika katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo amewataka washiriki hao kuimarisha uwazi ili mpango huo uweze kuwafikia walengwa katika maeneo yao ambao ni kaya masikini, kwani Wilaya ya Rombo zipo kaya nyingi zinazoishi katika hali ya umasikini.
Aidha amewataka washiriki wa warsha hiyo kutumia fursha hiyo kubadilishana uzoefu ambao utawasaidia katika kutekeleza majukumu yao.