TIMU ya mpira wa miguu ya Villa Squad ya Dar es Salaam iliyopanda daraja msimu huu Agosti 20 mwaka huu itaanza michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 kwa kucheza ugenini dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Mechi nyingine za raundi ya kwanza zitakuwa kati ya Coastal Union na Mtibwa Sugar (Mkwakwani, Tanga), Kagera Sugar na Ruvu Shooting (Kaitaba, Bukoba), Polisi Dodoma na African Lyon (Jamhuri, Dodoma) na Azam na Moro United (Chamazi, Dar es Salaam).
Raundi ya kwanza itamalizika Agosti 21 mwaka huu kwa mechi kati ya JKT Oljoro na Simba kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha na Yanga dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mzunguko wa kwanza (first leg) wa ligi hiyo utamalizika Novemba 5 mwaka huu wakati mzunguko wa pili (second leg) utamalizika Aprili Mosi mwakani ambapo jumla ya mechi 175 zitachezwa.
Pambano la watani wa jadi kati ya Yanga na Simba litafanyika Oktoba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi ya mzunguko wa pili ambapo Simba itakuwa mwenyeji itafanyika Aprili Mosi mwakani kwenye uwanja huo huo.