Wananchi: Tafiti za utawala bora za APRM zifanyiwe kazi


Ofisa Habari wa APRM Tanzania, Hassan Abbas

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wananchi wa kada mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya mjini Dodoma wamesema katika kuboresha na kuinua utawala bora nchini ni vyema Serikali ikafanyiakazi tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi zake hasa tafiti za utawala bora zinazofanywa na APRM.

Wananchi hao walitoa maoni hayo kwa nyakati tofauti walipotembelea banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

APRM ni Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora na hapa nchini taasisi hiyo imepewa dhamana ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu hali ya utawala bora ili kuisaidia Serikali kufanyiakazi changamoto zinazojitokeza.

“Nimesikia kuhusu utafiti wenu na hasa kuhusu namna nchi yetu inavyojenga uelewa wa wananchi ili waseme utawala bora wanaoutaka,”alisema mmoja wa wananchi waliohudhuria banda la APRM akijitambulisha kuwa ni mwanafunzi wa chuo cha Mipango huku akihoji kama ripoti za APRM na tafiti nyingine zinatekelezwa na Serikali.

Wananchi wengine walihoji kutaka kueleweshwa watashiriki vipi katika mchakato huo huku wengi zaidi wakionesha wasiwasi kama taasisi hiyo imketangazwa vya kutosha ili kuwapa nafasi wananchi.

Akifafanua baadhi ya kero za wananchi, Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw, Hassan Abbas alisema mchakato huo ulipoanza nchini wananchi walielimishwa kupitia mikutano iliyofanyika hadi vijijini na pia kupitia semina za makundi na vyombo vya habari.

“Kuhusu Serikali kufanyiakazi maoni ya wananchi hilo sisi bado hatujafikia hatua hiyo maana katika mchakato huu baada ya Rais kuwasilisha ripoti mbele ya wakuu wenzake wa Umoja wa Afrika ndipo anapewa michango kisha nchi inaanza kufanyiakazi maoni ya wananchi kwa miaka mitatu kabla ya kufanyika tena utafiti mwingine,” alisema.

Aliongeza kuwa hata hivyo kabla ya hatua hiyo kufikiwa nchi haizuiwi kuanza kufanyiakazi maoni ya wananchi wake yaliyotolewa katika ripoti. “Hapa nchini ukiangalia maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu masuala kama katiba na matakwa ya kudhibitiwa matumizi holela ya fedha katika chaguzi, haya yameshafanyiwa kazi au yanaendelea kufanyiwa kazi,” alisema Bw. Abbas.