BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) limetaka mapigano baina ya Israel na Wapalestina yakome katika Ukanda wa Gaza, na kuanza kwa mazungumzo ya amani kutafuta suluhisho la amani ya kudumu. Tangazo hilo lililoungwa mkono na wanachama wote 15 wa baraza hilo limezitaka pande hizo mbili kurejea katika makubaliano ya kusitisha uhasama ya Novemba, 2012 ambayo yalisimamiwa na Misri, ambayo hata hivyo hayaweki muda maalum wa utekelezwaji wake. Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour alisema kulingana na tafsiri yao kuhusu makubaliano hayo, usitishwaji wa mapigano unapaswa kuanza mara moja.
“Tunafuatilia kwa makini iwapo Israel itauheshimu wito huu (wa Baraza la UN) na tunatarajia kwamba itafanya hivyo, ikiwa watakwenda kinyume, basi tunazo hatua mbadala, na hatutalipa Baraza la Usalama muda wa kupumua,” alisema Mansour, na kuongeza kuwa ni jukumu la baraza hilo kushughulikia mchakato wa amani duniani, na kusimamisha ukandamizaji dhidi ya Wapalestina.
Idadi ya vifo kwa upande wa Wapalestina kutokana na mashambulizi ya Israel imepanda na kufika watu 157, na Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya robo tatu ya wahanga ni raia. Katika kile kinachoonekana kama kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa kutaka vita vikomeshwe katika Ukanda wa Gaza, Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Uingereza, William Hague pia ametoa wito wa kusimamishwa kwa mapigano na kusema atakutana na wenzake wa Marekani, Ufaransa na Ujerumani mjini Vienna Jumapili kuzungumzia suala hilo.
Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa amesema mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa ya kiarabu watakutana Jumatatu, katika kile alichokiita “juhudi zinazoendelea kukomesha ukandamizaji dhidi ya watu wetu”. Tangazo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo hata hivyo halina uzito kisheria, ndio tamko la kwanza kutoka baraza hilo lenye nguvu zaidi katika Umoja wa Mataifa, ambalo linakumbwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu mzozo kati ya Israel na Palestina.
Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel, imeitetea mashambulizi ya Israel kama jibu kwa maroketi yanayorushwa kwenye ardhi yake kutoka Ukanda wa Gaza ambao unadhibitiwa na chama cha Hamas. Wanachama wengine wote wa baraza hilo wamepinga mashambulizi ya Israel, ambayo mwakilishi wa Palestina amesema yameuwa watu 1000. Hakuna mtu yeyote aliyekufa kwa upande wa Israel kutokana na mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza.
Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema nchi yake inasimama pamoja na Israel na haki yake ya kujilinda, na kuongeza lakini kwamba hata Marekani inatiwa wasi wasi na kuzidi kuongezeka kwa mvutano, na ingependa juhudi zote zifanyike kuepusha vifo zaidi vya raia. Tangazo la Umoja wa Mataifa haliyataji bayana mashambulizi ya maroketi yanayofanywa na Hamas, wala mashambulizi ya Israel kama jibu kwa maroketi hayo.
-DW