Salma Kikwete Apinga Ndoa za Utotoni na Taasisi ya Segal Family

Mwanzilishi wa Taasisi ya Segal Family, Barry Segal akimpongeza Mke wa Rais Mama Salma Kikwete mara baada ya kutoa hotuba ya kusisimua kwenye mkutano wa mwaka wa Taasisi hiyo tarehe 10.7.2014.

Mwanzilishi wa Taasisi ya Segal Family, Barry Segal akimpongeza Mke wa Rais Mama Salma Kikwete mara baada ya kutoa hotuba ya kusisimua kwenye mkutano wa mwaka wa Taasisi hiyo tarehe 10.7.2014.

Mke wa Rais na Mwenyeiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete akizungumza na Barry Segal, Mwanzilishi wa Taasisi ya Segal Family ya nchini Marekani wakati walipokutana kwenye mkutano wa mwaka wa Taasisi hiyo ya kimarekani uliofanyika katika hoteli ya Ngurdoto huko Arusha tarehe 10.7.2014. PICHA ZOTE NA JOHN  LUKUWI. 

Mke wa Rais na Mwenyeiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete akizungumza na Barry Segal, Mwanzilishi wa Taasisi ya Segal Family ya nchini Marekani wakati walipokutana kwenye mkutano wa mwaka wa Taasisi hiyo ya kimarekani uliofanyika katika hoteli ya Ngurdoto huko Arusha tarehe 10.7.2014. PICHA ZOTE NA JOHN  LUKUWI. 


Na Anna Nkinda – Maelezo, Arusha

JAMII imetakiwa kushirikiana kwa pamoja kupiga vita ndoa za utotoni hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa sera na sheria za kuwalinda watoto zinafuatwa ili watoto wa kike waweze kusoma na kumaliza masomo yao kama ilivyo kwa watoto wa kiume. Mwito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizungumza na viongozi na Asasi za kiraia kutoka nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaohudhuria mkutano wa mwaka wa siku nne wa Taasisi ya Familia ya SEGAL unaofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto mjini Arusha.
 
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema ndoa za utotoni ni moja ya sababu inayowafanya watoto wa kike kutomaliza masomo yao kwani idadi ya wanafunzi wa kike walioko shule ya msingi ni kubwa lakini katika elimu ya Sekondari idadi yao inapungua ukilinganisha na watoto wa kiume.
 
“Tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonyesha kuwa katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika asilimia 24 ya wasichana wanaolewa wakiwa na umri mdogo wa kati ya miaka 15 hadi 18, kwa umri huu watoto hawa wanatakiwa kuwa shule za Sekondari na siyo kuishi maisha ya ndoa wakiwa wameolewa.
 
Kutokana na sababu hii tunatakiwa kuunganisha nguvu zetu ili kuhakikisha katika nchi zetu kuna sera na sheria ambazo zitawalinda wasichana wadogo dhidi ya wanaume wabaya, wakati huo huo tunatakiwa kushirikiana na jamii ili iweze kuwajengea mazingira mazuri na salama ambayo yatawalinda watoto hawa,” alisema Mama Kikwete.

Baadhi ya washiriki kwenye mkutano wa mwaka wa Taasisi ya Segal Family wakisikiliza hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwenye ukumbi wa Ngurdoto tarehe 10.7.2014.

Baadhi ya washiriki kwenye mkutano wa mwaka wa Taasisi ya Segal Family wakisikiliza hotuba iliyokuwa ikitolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwenye ukumbi wa Ngurdoto tarehe 10.7.2014.


Aidha Mama Kikwete alisema mkutano huo umekuja wakati muafaka kwani nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto ya maambukizi makubwa ya Virusi Vya Ukimwi (VVU)  miongoni mwa vijana. Kazi kubwa imefanywa ili kuhakikisha maambukizi ya ugonjwa huo yanapungua ila hata hivyo bado kuna vijana wengi ambao hawafikiwi na hudumu muhimu wanazozihitaji.
 
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema, “Ugonjwa huu bado ni tatizo katika nchi zetu kati ya maambukizi mapya 620,000 yanayotokea kila mwaka barani Afrika kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 asilimia 60 ni wasichana. Hii inamaana kuwa kwa kila saa moja wasichana 31 wanapata maambukizi kwa kila vijana wa kiume 21 tunahitajika kufanya jambo la ziada hasa kwa wasichana ili kukabiliana na jambo hili.
 
Vijana wanatakiwa kufundishwa afya ya uzazi ili waweze kujilinda na kuweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu miili yao hii ni moja ya silaha ambayo itawalinda wasichana. Najua katika jamii nyingi ni vigumu kwa wazazi kuongea jambo hili na watoto wao na kuona kuwa ni mwiko, naamini muda umefika kuangalia tamaduni hizi kwani watoto wengi wanapoteza maisha kutokana na jamii kukaa kimya,”.
 
Alisema wao kama wazazi hawatakubali kuona watoto wao wanajihusisha na mahusiano ya kimapenzi wangali wadogo, wanapata mimba wakiwa na umri mdogo na kukatisha masomo yao kwani ni wajibu wao kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kuhakikisha kuwa hawapati maambukizi ya Ukimwi.
 
Kwa upande wake mwanzilishi wa Taasisi hiyo Barry Segal alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania na kumuahidi kuwa watashirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa matatizo yanayowakabili yanapungua au kuisha kabisa.

Alisema Taasisi hiyo imeamua kufanya kazi na WAMA ili kuhakikisha kuwa kampeni ya Mtoto wa Mwenzio ni Mwanao inatekelezwa hapa nchini hii itasaidia jamii kuwajengea mazingira ya kuwalinda vijana wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24 na kuwalinda na mazingira hatarishi ambayo yanaweza kuwapelekea kupata maambukizi ya VVU na hivyo kupata kizazi kisicho na maambukizi .

Taasisi ya Familia ya SEGAL ambayo makao yake Makuu yapo nchini Marekani wanashirikiana na kufanya kazi na asasi mbalimbali za Kiraia zinazofanya kazi za kijamii ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake, kupiga vita mimba za utotoni zilizopo nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.