Wafanyabiashara wa vitunguu saumu eneo la Kariakoo
Na Mwandishi Wetu
WAFANYABIASHARA wasambazaji wa vitunguu saumu jijini Dar es Salaam wameulalamikia utaratibu mpya wa tozo za ushuru kwa bidhaa hiyo, unaofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, ambao umepandisha kodi kwa kiasi kikubwa tofauti ilivyokuwa awali.
Malalamiko hayo yametolewa jana jijini Dar es Salaam kwenye soko la wafanyabiashara hao eneo la Kariakoo, walipokuwa wakifanya mahojiano kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi.
Akizungumza mmoja wa wafanyabiashara hao, Ally Karatu alisema Halmashauri ya Mbulu kwa sasa imewapandishia ushuru ghafla kutoka sh. 1500 iliyokuwa ikilipwa awali hadi kufikia sh. 15,000 kwa gunia jambo ambalo linawaathiri kwa kiasi kikubwa hivi sasa.
Alisema kitendo cha kupandishwa kwa ushuru huo kumewaathiri kwa kiasi kikubwa kwani kimeongeza mzigo wa gharama za usafirishaji, ambazo kwa sasa pia zimepanda kutokana na kupanda kwa bei ya nishati za mafuta ya dizeli na petroli.
Naye mfanyabiashara mwingine, Cosmas Steven alisema kitendo cha kupanda kwa kodi hiyo tena bila wao kushirikishwa huenda kikawaathiri wakulima wa zao hilo ndani ya Halmashauri ya Mbulu, kwani tayari baadhi wameanza kukata tamaa nakufikiria kufuata maeneo mengine ambayo ushuru upo chini.
“Mi nafikiri ni bora wangetushirikisha na kuangalia nini cha kufanya kabla ya wao kupandisha ushuru, unajua zao hili kwanza tunapata shida sana, kwanza halidumu muda mrefu…sasa tunapotumia gharama kubwa mwisho unaweza usiambulie chochote na kukuta linaharibikia sokoni,” alisema Steven.
Hata hivyo akijibu malalamiko hayo jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbulu, Simon Mayeye alisema kiwango cha ushuru wa sh. 15,000 kwa gunia kinacholalamikiwa na wafanyabiashara hao ndicho kilichopitishwa na Serikali, hivyo kitaendelea kutozwa.
Alisema awali kabla ya maelekezo yaliopitishwa katika bajeti mpya 2011/2012 walikuwa wakitoza kwa makadirio jambo ambalo liliwazoesha vibaya wafanyabiashara hao. “Unajua huenda wao hawajaelewa hicho ndio kiwango halali…tumeelekezwa kuwa ili kuongeza mapato ya Serikali ushuru wa mazao usizidi asilimia tatu ya bei ya kununulia. Na ukiangalia hivi karibuni walikuwa wakinunua debe la vituguu hivyo sh. 100,000 na asilimia tatu yake ni sh. 3,000, gunia lina madebe matano ukizidisha unapata sh. 15,000…kiwango hiki ni sahihi,” alisema Mkurugenzi Mayeye.