CCM sasa ‘yaingilia’ utendaji wa EWURA

Na Joachim Mushi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezipinga sababu zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA), za kupandisha kodi ya mafuta ya taa kwa kisingizio cha kudhibiti vitendo vya uchakachuaji vilivyokuwa vimeshamiri.

Madala CCM imeiagiza Serikali kuhakikisha inatafuta njia za kushusha bei ya mafuta ya taa nchini, kwa kuwa ndiyo nishati inayotumiwa na wananchi wengi hasa wenye kipato cha chini.

Kauli hiyo imetolewa Agosti Mosi na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Mnauye mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kilichomalizika mjini Dodoma, ambacho kimejadili masuala mbalimbali yanayolikabili Taifa.

Katika taarifa hiyo, Nape amesema, Kamati Kuu ya CCM haijaridhishwa na kiwango cha kupanda kwa bei ya mafuta ya taa nchini kwa kuwa ndio nishati inayotumiwa na wananchi wengi wenye kipato cha chini.

“Aidha Kamati Kuu haikuridhishwa na maelezo ya kupandishwa kwa bei ya mafuta hayo kwa kisingizo cha kuzuia uchakachuaji wa mafuta mengine. Hivyo basi, Kamati Kuu imeiagiza Serikali kutafuta njia za kushusha bei ya mafuta ya taa na kuvitaka vyombo vya Serikali vinavyohusika na usimamiaji wa ubora wa mafuta, vihakikishe vinatimiza wajibu wake kuzuia kabisa mtindo wa uchakachuaji wa mafuta nchini na si kupandisha bei ya mafuta ya taa kama suluhisho,” amesema Nape katika taarifa hiyo.

Aliongeza kuwa Kamati Kuu pia imeguswa na tatizo la umeme nchini kwani athari zake kwa uchumi wa Taifa na mtu mmoja mmoja ni kubwa. Hivyo imeitaka Serikali kutumia muda uliotolewa kurekebisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini na kuja na mpango wa dharura wa kunusuru hali hiyo na kulimaliza kabisa tatizo la umeme nchini.

Hata hivyo maagizo ya CCM yanapingana na Ewura ambayo hivi karibuni ilifanya mabadiliko na kuongeza kodi ya mafuta ya taa kwa madai hatua hiyo itadhibiti vitendo vya uchakachuaji wa mafuta ikiwemo diseli.

Katika mabadiliko hayo, EWURA ilipandisha kodi ya mafuta ya taa kwa waagizaji wa nje kutoka sh. 52 hadi sh. 400.30, ikiwa ni kudhibiti udanganyifu ambao ulikuwa ukifanywa na baadhi ya waagizaji wasiowaaminifu.

Hata hivyo katika ufafanuzi wake juu ya mabadiliko hayo iliweka wazi kuwa mabadiliko hayo hayata muathiri mtumiaji wa mafuta ya taa kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Ewura ilisema awali kabla ya mabadiliko baadhi ya waagizaji walikuwa wakiagiza mafuta ya taa kwa wingi kwa ajili ya uchakachuaji kutokana na urahisi wa bidhaa hiyo kwa kodi tofauti na nishati za mafuta mengine.

Mbali na EWURA kupandisha kodi hiyo ili kudhibiti vitendo vya uchakachuaji iliamua kuweka punguzo la sh. 224.50 ikiwa ni kinga kwa mtumiaji wa mwisho yaani mwananchi hali ambayo haitamuathiri mtumiaji huyo.