WANAMGAMBO wa Al Shabaab wamedai kuwa wamemuua kwa kumfyatulia risasi mbunge maarufu mjini Mogadishu. Taarifa zinasema, Ahmed Mohamud Hayd (Mb) aliuawa baada ya kutoka hotelini ambapo katika tukio hilo, mlinzi wake pia aliuawa huku Katibu wa Bunge akibaki amejeruhiwa.
Kundi la Al-Shabaab, ambalo lina uhusiano na lile la al-Qaeda, limeapa kuendelea na mashambulizi zaidi katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wanamgambo hao walipoteza ngome yao mjini Mogadishu na kuchukuliwa na Vikosi vya Umoja wa Afrika mwaka 2011, lakini wameendelea na mashambulizi ya mabomu na mauaji mjini humo.
Msemaji wa kundi hilo, Abdulaziz Abu Musab alisema kuwa kundi lake limemuua kama ilivyopangwa na kuwa wataendelea kuwafuatilia wabunge wengine ikiwa hawataachana na Bunge nchini humo. Al-Shabaab imekua ikipigania kuunda taifa la kiislamu nchini Somalia.
-BBC