JK Aufagilia Uhusiano Kati ya Afrika Kusini na Tanzania

Bendera za Tanzania na Afrika Kusini

Bendera za Tanzania na Afrika Kusini


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesifia uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini akisema kuwa uhusiano huo haujapata kuwa mzuri zaidi ya ulivyo sasa. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni muhimu kwa Afrika Kusini kuendelea kuonyesha uongozi katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa sababu kwa kufanya hivyo Afrika Kusini itakuwa inatimiza jukumu lake la kihistoria.

Rais Kikwete alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam wakati anaagana na Balozi wa Afrika Kusini katika Tanzania, Thanduyise Henry Chiliza ambaye amemaliza muda wake wa utumishi nchini. Rais Kikwete alimwambia Balozi huyo kuwa ni nchi chache dunia kwa sasa ambazo zina uhusiano wa karibu zaidi na Tanzania kuliko Afrika Kusini.

“Tumekuwa washirika wa karibu sana katika uhusiano wa kikanda na uhusiano wa kimataifa. Uhusiano wetu haujapata kuwa wa karibu zaidi ya sasa katika historia. Tunakushukuru Mheshimiwa Balozi kwa mchango wako katika kuimarisha uhusiano wetu kiasi hicho.”
Rais Kikwete pia amesifia mchango wa Afrika Kusini katika utulivu ulioko katika eneo la Kusini kwa Afrika akisema kuwa anatambua mchango na uongozi wa nchi hiyo katika hali hiyo.
“Tunatambua uongozi wa Afrika Kusini katika eneo letu la Afrika. Ni jukumu la kihistoria la nchi hiyo ambalo Afrika Kusini lazima iendelee kulitimiza kwa kiwango kinachotarajiwa na sisi wote.”
Naye Balozi Chiliza amemshukuru Rais Kikwete kwa kumuunga mkono wakati wa uwakilishai wake na hivyo kumsaidia kutimiza majukumu yake ya kibalozi.
“Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ushauri na maelekezo yako ya kiuongozi wakati wa utumishi wangu katika Tanzania. Bila kunisaidia pengine kazi yangu ingekuwa ngumu zaidi.”