Pinda Awataka Viongozi wa Dini Kuombea Uchaguzi Serikali za Mitaa

Waziri Mizengo, Pinda akiwa na baadhi ya viongozi wa dini.

Waziri Mizengo, Pinda akiwa na baadhi ya viongozi wa dini.


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini kote nchini na wananchi waungane pamoja ili kuombea uchaguzi mkuu wa viongozi wakuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Ametoa wito huo Julai mosi, 2014 wakati akizungumza na maelfu ya waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarsicius Ngalalekumtwa katika uwanja wa Kichangani wa Kanisa Kuu la Kihesa.

“Maaskofu wote mliopo hapa, najua mnavyoipenda Tanzania… kila kanisa lina sala maalum ya kuliombea Taifa na viongozi wake, ninawaomba viongozi wetu mliombee Taifa letu ili mambo yaende salama na hasa uchaguzi wa mwakani,” alisema.

Akirejea mahubiri yaliyotolewa kwenye ibada hiyo na Mhashamu Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo Katoliki la Tabora ambaye alitoa mfano wa Daudi na Goliathi, Waziri Mkuu alimfananisha Goliathi na masuala ya rushwa, ubinafsi na tabia ya viongozi kutojali wananchi wa hali ya chini.

“Viongozi tusipokuwa waadilifu, tukawa wala rushwa na hatujali wananchi wa hali ya chini tutakuwa sawa na Goliathi. Nawasihi sana ombeeni Taifa hili na uchaguzi mkuu ujao ili Mungu atupe Daudi atakayeweza kuliongoza Taifa hili na kulipeleka kunakostahili,” alisema huku akishangiliwa.

Waziri Mkuu ambaye alihudhuria sherehe hizo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, ametumia fursa hiyo pia kuwaomba wote kwa pamoja waendelee kuliombea Taifa katika kipindi hiki cha mchakato wa kuandaa Katiba Mpya. “Watanzania wote tuwe na moyo wa kuvumiliana na kupendana. Tumuombe Mungu atuwezeshe kupata Katiba mpya katika hali ya maelewano na amani. Tuombee Taifa na tuombee Watanzania ili tusije tukatoka katika mstari.”

Alisema ushauri uliotolewa na Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severini Niwemugizi wa kuwataaka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba warejee mara moja ni wa muhimu. “Ushauri wa Baba Askofu ni wa makini, turudi tukabishane pale ndani, lakini pamoja na yote sheria inasema mwamuzi wa mwisho ni Watanzania kupitia kura ya maoni. Wale tuliopewa dhamana ya kupitia rasimu turudi pale tuikamilishe ili Watanzania waweze kupata fursa ya kupiga kura ya maoni,” alisema.

Mapema, akiwasilisha salamu kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severini Niwemugizi wa Jimbo la Ngara aliwataka wajumbe wa Bunge maalum la Katiba kurejea kwenye mkutano wake uliopangwa kuanza Agosti 5, mwaka huu.

“Ninatumia neno kuwataka na siyo kuwaomba warejee bungeni mwezi ujao. Wasipofanya hivyo au kufanya mizengwe mingine na kutupatia Katiba isiyotufaa, nitawaomba Watanzania wote tuweke uzalendo mbele na kuikataa rasimu ya Katiba itakayoletwa na pia tuwanyime uongozi katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.

Aliwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi wakati wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura. “Watanzania tuna tabia ya kudharau siasa. Tusidharau masuala ya siasa kwa sababu ni muhimu na yanagusa maisha yako na yangu, yanagusa maisha ya watoto wako,” alisema.

Sherehe hizo za jubilei ya miaka 25, zilihudhuriwa na maaskofu 19 kutoka majimbo mbalimbali ya kanisa katoliki hapa nchini, wawakilishi wa maaskofu watatu na abate mmoja. Viongozi wa kitaifa waliohudhuria ni Spika wa Bunge, Mama Anne Makinda; Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa; Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na baadhi ya wabunge wa mkoa wa Iringa.

Askofu Ngalalekumtwa (66) alipata upadrisho Aprili 7, 1973 huko San Ginesio, Camerino, nchini Italia na kupata daraja ya uaskofu mwaka 1988 ambapo alisimikwa rasmi Januari 1989 kuwa Askofu wa Jimbo la Sumbawanga.