RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Juni 24, 2014, amewaapisha Wajumbe na Katibu wa Tume ya Kuchunguza Operesheni Tokomeza katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam. Aidha, Rais Kikwete amemwapisha Ofisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje, Bwana Joseph Edward Sokoine kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Wajumbe wa Tume ya Tokomeza walioapishwa ni Jaji Mstaafu Hamisi Amiri Msumi ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo na Majaji Wastaafu Stephen Ernest Ihema na Vincent Damian Lyimo ambao wanakuwa wajumbe wa Tume hiyo. Katibu wa tume hiyo ambaye pia ameapishwa na Rais Kikwete ni Bwana Frederick Kapela Manyanda.
Wajumbe pamoja na Katibu wa tume waliteuliwa karibuni na Rais Kikwete ili kuchunguza kwa nia ya kupatikana ukweli wa jinsi Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa kufuatia malalamiko yaliyotokana na Operesheni hiyo ambayo ililenga kukabiliana na ujangili wa wanyamapori nchini.
Serikali ilisimamisha Operesheni hiyo kufuatia malalamiko yaliyoanzia Bungeni mwaka jana lakini bado Rais Kikwete aliliambia Bunge hilo hilo Novemba mwaka jana kuwa Operesheni hiyo itaanzishwa tena baada ya kufanyika uchunguzi wa kubaini mapungufu ya ile ya kwanza.
Naye Bwana Sokoine ambaye alikuwa Ofisa Balozi Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Canada aliteuliwa karibuni pia kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Dorah Msechu ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania katika Sweden.