Serikali Yamchunguza Aliyepewa Zawadi ya Mke Kijijini

Mkuu Shirika la Habari la Serikali SABC, Hlaudi Motsoeneng (katikati)  akipiga picha na binti aliyepewa kama zawadi.

Mkuu Shirika la Habari la Serikali SABC, Hlaudi Motsoeneng (katikati) akipiga picha na binti aliyepewa kama zawadi.

Picha ya pamoja mara baada ya mke kukabidhiwa.

Picha ya pamoja mara baada ya mke kukabidhiwa.

TUME inayohusika na masuala ya usawa wa kijinsia nchini Afrika Kusini inafanya uchunguzi kuhusu madai kuwa Mkuu wa Shirika la Habari la SABC nchini humo alikabidhiwa msichana mwenye umri wa miaka 23 kama zawadi awe mkewe.

Tume hiyo imesema kuwa imepokea malalamiko kwamba viongozi wa kitamaduni walimkabidhi Mkuu Shirika la Habari la Serikali SABC, Hlaudi Motsoeneng mke kama zawadi jambo ambalo watetezi wa haki wa masuala ya kijinsia hawakubaliani nalo. Viongozi hao walikuwa sehemu ya kikundi cha wazee wa kitamaduni waliokuwa wanataka vipindi zaidi vya lugha yao kupeperushwa kwenye televisheni hiyo hivyo huwenda walichokifanya ni kama rushwa.

Serikali imesema imechukizwa na tukio hilo na kwamba inashangaa ni kwa vipi jambo hilo limetokea. Tukio hilo linasemekana kutokea wakati wa ziara ya hivi karibuni ya Hlaudi Motsoeneng katika Mkoa wa Limpopo Kaskazini mwa nchi hiyo ambako yeye na maofisa wengine wakuu walikutana na wazee hao.

Taarifa ya serikali ilisema; “Tabia ya kutumia wanawake kama zawadi na kufananishwa na mifugo wanaotolewa kama zawadi wakati msichana anapoolewa ni utamaduni usio kubalika na ni kinyume cha haki za binadamu na pia ni kama matusi kwa demokrasia na uhuru wa watu.

Takriban wasichana 10 waliorodheshwa mbele ya maofisa hao huku wakitakiwa kuchagua. Bwana Hlaudi Motsoeneng alichagua mwanamke mmoja ambaye alimfurahisha. Hata hivyo wasichana wote waliambatana na wazazi wao na walifahamu kila kilichokuwa kinaendelea na inaarifiwa kuwa wote walikubali.

Kwa mujibu wa jarida Sowetan, Motsoeneng alichagua msichana aliyekuwa na umri wa miaka 23 ambaye pia ni mwanafunzi. Alipigwa picha akiwa kifua uchi akisimama kando yake. Pia inaarifiwa alikabidhiwa Ng’ombe na Ndama.

Wizara ya masuala ya wanawake nchini humo, ilisema tabia hiyo ni hujuma kwa utamaduni; “Tabia ya kutumia wanawake kama zawadi ungedhani ni n’gombe, bila shaka ni hujuma kwa utamaduni,” ilisema taarifa ya wizara hiyo.

Msemaji wa kituo cha SABC, Kaizer Kganyago, alisema hajapokea habari yoyote kuhusu uchunguzi unaofanywa na tume hiyo na kwamba ikiwa ina swali lolote kuhusiana na tukio hilo, inapaswa kuhoji viongozi hao wa kitamaduni. Huku Msemaji wa Tume, Javu Baloy akisema ujumbe tayari umewasilishwa kwa wote waliohusika na mapendekezo ya adhabu yatatolewa mwezi ujao.