Na Mwandishi Maalum, Santa Cruz, Bolivia
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal amezitaka nchi wanachama wa G77+China, kuhakikisha zinaboresha kilimo ili ziwe na hifadhi ya kutosha ya chakula kwa wananchi wake.
Akihutubia mkutano wa mwaka kwa nchi za G77+China ambao pia ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya umoja wa nchi hizi, unaofanyika jijini St Cruz De Sierra, Dkt Bilal alisema nchi za umoja huu zina maeneo mazuri kwa kilimo na hivyo ni muhimu kuyatumia maeneo haya katika kuzalisha chakula kwa lengo la kuhifadhi na kuwa na usalama wa chakula nyakati zote.
Dk. Bilal alisema, nchi hizi kwa pamoja zinahitaji kuwa na kauli moja kuhusu masharti yanayowekwa na nchi kubwa hasa katika kilimo na kuelezea kuwa ili mafaniio makubwa yapatikane, lazima uwepo uwekezaji wa ndani katika kilimo sambamba na serikali za nchi hizi kuchangia shughuli za uzalishaji ili kuwa na kilimo chenye tija kwa wakulima na kinachoweza kuchangia usalama wa chakula.
Kuhusu suala la mazingira, Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwaeleza wajumbe wa G77+China kuwa, maazimio yaliyofikiwa Rio+20 na mapendekezo kuhusu ‘Kesho tunayoitaka’ yanazihitaji nchi hizi kupaza sauti zake kwa pamoja kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani suala hili kwa sasa haliwezi kutatuliwa na nchi moja bali linahitaji nguvu ya kila mtu duniani.
Makamu wa Rais alifafanua kuwa bila kuwa na mazingira bora maendeleo endelevu yatabakia ndoto na pia kufanikisha Malengo ya Milenia kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa itakuwa vigumu kama suala la mazingira litaachwa kwa kila nchi kufanya inavyotaka.
“Kundi hili lina kazi kubwa iliyo mbele yetu na hasa kuhusu malengo mapya ya maendeleo baada ya kukamilika kwa muda wa Malengo ya Milenia mwakani. Tunahitajika kubuni njia za kuzipatia nchi zetu maendeleo katika Nyanja za uchumi, kijamii na mazingira ili tufanikiwe vema,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Katika hotuba hiyo Mheshimiwa Makamu wa Rais pia alizungumzia kuhusu umuhimu wa nchi hizi kuweka msisitizo wa kuwapa wananchi maji safi na salama, umuhimu wa kuwa na nishati inayotosheleza matumizi ya uzalishaji, uwepo wa huduma bora za afya na elimu ili kupiga hatua kwa haraka baina ya wananchi wa nchi hizi. “Nafahamu kufanikisha haya yote ni kazi kubwa lakini hatuna muda wa kusubiri. Ni lazima tufanye kazi ili kubadili hali iliyopo,” alifafanua.
Mkutano huo ambao umekamilika jana kwa mwenyeji wake Rais Evo Morales kuwashukuru wanachama wa G77+China walioweza kushiriki mkutano huo, pia ulionesha nia kwa wanachama wa nchi hizi kutafuta majibu ya changamoto ya ukosefu wa ajira unaokabili wananchi wengi wa nchi hizi. Viongozi wengi walisisitiza kuwa, suala la ajira hasa kwa vijana linatakiwa kutazamwa upya na hasa ukizingatia rasilimali zilizopo katika nchi za G77+China ili zitumike katia kutengeneza ajira mpya zitakazoweeza kusaidia kuboresha maisha ya watu wa nchi hizi kwa miaka mingi ijayo.