MTU mmoja amefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa baada ya kurushiwa bomu na watu wasiojulikana katika eneo la Darajani, muda mfupi baada ya kuhudhuria mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Sheikh Kassim Mafuta Kassim (38) mkazi wa Pongwe mkoani Tanga.
Tukio hilo limejiri saa 2:30 usiku na bomu hilo lilirushwa kwa mkono na watu wasiojulikana wakati waumini wakiagana na mtoa mawaidha Sheikh Kassim katika eneo la kuegesha magari Darajani visiwani Zanzibar. Aliyefariki dunia kwa bomu hilo ametajwa ni Muhammed Khatib Mkombalaguha, ambaye ni mwanafunzi wa Sheikh Kassim.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI), Yusuph Ilembo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na tayari Jeshi la Polisi limeanzisha operesheni maalumu ya kuwasaka watu waliohusika na shambulio hilo kwa kushirikiana na vikosi vingine vya ulinzi na usalama visiwani hapa.
“Mlipuko pia umesababisha magari mawili yaliyokuwepo katika eneo la tukio kuathirika, ikiwemo kupasuka mipira na gari lingine kuvunjika kioo, na tayari tumeanza kufanya uchunguzi ingawa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa hadi hivi sasa,” alisema DDCI Ilembo.
Alisema magari yaliyoathirika ni Toyota Prado ambalo alikuwa akitumia Sheikh Kassim Mafuta tangu alipowasili visiwani Zanzibar, Jumatatu ya wiki hii na kutoa mawaidha katika misikiti mbalimbali ya kisiwani Unguja pamoja na Toyota IST.
Alisema katika eneo la tukio kumekutwa mabaki ya mlipuko ambayo tayari yameanza kufanyiwa uchunguzi na wataalamu wa mabomu, kubaini kama mabomu hayo ni ya kienyeji ama yalitengenezwa kiwandani.
Aliwataja majeruhi ni Sheikh Kassim Mafuta, Kassim Issa Muhammed (38) mkazi wa Fuoni, Hamad Nassor Kassim (46), Khelef Abdallah Abdallah (21), Khalid Ahmed Haidar (16) na baba yake mzazi Ahmed Haidar Jabir (47) mkazi wa Kiembesamaki ambao wamelazwa katika hospitali ya Alrahma iliyopo Kilimani na Suleiman Ali Juma ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita.
Kwa mujibu wa Kamanda Ilembo waathirika wana majeraha makubwa, huku mabaki ya vipande vya mabomu vikitolewa kwenye miili yao. Alisema Khalid Ahmed Haidar ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Light Academic iliyopo Nairobi ametolewa vipande sita.
“Tumeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuchukua tahadhari, ikiwamo kufanya doria na tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za siri zitakazosaidia kuwakamata waliohusika,” alisema DDCI Ilembo.
Akizungumza na gazeti hili katika Hospitali ya Alrahma, baba wa marehemu Muhammed Khatib Mkombalaguha, alisema alipokea taarifa za kifo cha mwanaye kupitia kwa ndugu yao anayeishi Arusha na baadaye alithibitishiwa kutokea kwa tukio hilo baada ya kuwasiliana na Sheikh Abdulrahman Mussa anayeishi katika eneo la Jitengeni Pongwe, mkoani Tanga.
“Tulianza safari saa 4:00 usiku kupitia Dar es Salaam, na saa 12:00 alfajiri tulifanikiwa kufika bandarini na kuanza safari ya Zanzibar, marehemu ana mke na watoto wawili,” alisema baba wa marehemu.
CHANZO; Mwananchi