Bajeti 2014/15 Maumivu kwa Walevi, Wafanyakazi Wapunguziwa Kodi

Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum akiwasilisha hotuba ya mapendekezo ya  Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/2015 leo Bungeni mjini Dodoma.

Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum akiwasilisha hotuba ya mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/2015 leo Bungeni mjini Dodoma.

Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum akisindikizwa na askari wa Bunge kwenda kusoma Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015 leo Bungeni mjini Dodoma.

Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum akisindikizwa na askari wa Bunge kwenda kusoma Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015 leo Bungeni mjini Dodoma.


*Sigara, Juisi, Mvinyo Vyapanda Tena, Wastaafu wakumbukwa

Na Joachim Mushi

WAZIRI wa Fedha leo mjini Dodoma amesoma Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2014/15 ambapo bajeti hiyo ikiendelea kuwakamua watumiaji wa vileo (walevi), wapenda starehe pamoja na wavutaji wa sigara huku safari hii hauweni ikijitokeza kwa wafanyakazi baada ya kupunguza kodi za mishahara.

Akisoma bajeti hiyo, Bungeni mjini Dodoma Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum (Mb) alisema ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka nchini na ambayo haijaoteshwa imepanda kutoka shs 341 kwa lita hadi shs 375, huku ushuru wa bia nyingine kutoka shs 578 kwa lita hadi shs 635.

Alisema ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu ya nchini kiwango kinachozidi asilimia 75 imeongezeka kutoka shs 160 kwa lita hadi shs 176, ushuru wa mvinyo wa nje kiwango kinachozidi asilimia 25 umepanda kutoka shs 1,775 kwa lita hadi shs 1,953, huku ushuru wa vinywaji vikali ukipanda kutoka shs 2,631 kwa lita hadi shs 2,894.

“…Viwango vya ushuru wa Bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo; Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 9,031 hadi shilingi 11,289 kwa sigara elfu moja. Hii ni sawa na ongezeko la shilingi 2,258 kwa sigara elfu moja au shilingi 2.25 kwa sigara moja,”

“…Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 21,351 hadi shilingi 26,689 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 5,338 au shilingi 5.30 kwa sigara moja. Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 38,628 hadi shilingi 48,285 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la shilingi 9,657 sawa na shilingi 9.65 kwa sigara moja,” alisema Waziri Salum.

Aidha alisema ushuru wa vinywaji baridi umepanda kutoka shs 91 kwa lita hadi shs 100 na bidhaa za maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ya nchini imeongezeka kutoka shs 9 kwa lita hadi shs 10, ushuru wa bidhaa za maji ya matunda (juisi) inayozalishwa nje ya nchini imepanda kutoka shs 110 kwa lita hadi shs 121. Aliongeza tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara imepanda kutoka shs 19,510 hadi 24,388 kwa kilo, ushuru wa “cigar” unabaki kuwa asilimia 30.

Alisema mabadiliko hayo ya tozo za ushuru wa bidhaa kwa pamoja yanatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shs milioni 124,292.0, huku pia waziri akipendekeza sheria ya Ushuru wa Mafuta, Sura 220 kufanyiwa marekebisho ili kuondoa mamlaka ya Waziri wa Fedha.

Akisoma vipaombelea katika sekta mbalimbali Waziri Salum alisema sekta ya Nishati na Madini imetegewa jumla ya shs bilioni 1,090.6 zimetengwa, shilingi bilioni 290.2 zimetengwa kwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwa ajili ya vijijini, shilingi bilioni 80 zikitengwa kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa miundombinu ya usafirishaji imetengewa shs bilioni 2,109.0, ambapo shs bilioni 179.0 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa na ukarabati wa reli ya kati na bilioni 1,414.8. Kilimo kimepewa jumla ya shs bilioni 1,084.7 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya SAGCOT.

Kwa upande wa sekta ya elimu; jumla ya shs bilioni 3,465.1 zimetengwa, ambapo bilioni 307.3 zita gharamia mikopo ya elimu ya juu. Aidha Serikali itaendelea kuimarisha ubora wa elimu ikijumuisha miundombinu ya elimu, huku akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia upatikanaji vifaa vya kujifunzia.

“Sekta ya Maji; jumla ya bilioni 665.1 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa visima katika vijiji 10 kwa kila Halmashauri na kukamilisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dk. Servacius Likwalile (wa tatu kushoto mstari wa pili kutoka nyuma), Maafisa wakuu wa Serikali na baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia kwa makini hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015 leo Bungeni mjini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dk. Servacius Likwalile (wa tatu kushoto mstari wa pili kutoka nyuma), Maafisa wakuu wa Serikali na baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia kwa makini hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015 leo Bungeni mjini Dodoma.


Aidha aliongeza kuwa sekta ya Afya imetengewa jumla ya shs bilioni 1,588.2 kwa ajili ya ununuzi wa madawa, kuzuia magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti UKIMWI na Malaria. Sekta ya utawala Bora zimetengwa jumla ya bilioni 579.4 kwa ajili ya kuimarisha utawala bora ikijumuisha kugharamia Bunge Maalum la Katiba.

“…Mheshimiwa Spika, ili kuziba nakisi ya bajeti, Serikali inatarajia kukopa kutoka katika vyanzo vya ndani na nje shilingi bilioni 4,275.2. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 2,265.7 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na mkopo wa ndani shilingi bilioni 689.6 ambao ni asilimia 1.1 ya Pato la Taifa na shilingi bilioni 1,320 ambazo ni mikopo yenye masharti ya kibiashara zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema.

“…Jumla ya shilingi bilioni 19,853.3 zimekadiriwa kutumika katika mwaka 2014/15, kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni shilingi bilioni 13,408.2 ambayo yanajumuisha shilingi bilioni 5,317.6 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, Wakala na Taasisi za Serikali,”

“Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi bilioni 4,354.7, na Matumizi Mengineyo shilingi bilioni 3,735.9, jumla ya shilingi bilioni 6,445.1 sawa na asilimia 33 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Aidha, asilimia 69 ya fedha za maendeleo zitagharamiwa na fedha za ndani ambayo ni shilingi bilioni 4,425.7.

“Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 689.6 zinatokana na mkopo kutoka vyanzo vya ndani, shilingi bilioni 1,320 ni mikopo ya masharti ya kibiashara, shilingi bilioni 375.5 ni mikopo ya kibajeti, na shilingi bilioni 2,040.6 inatokana na mapato ya ndani. Kiasi cha shilingi bilioni 2,019.4 kitagharamiwa kwa fedha za nje, misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha Mifuko ya Kisekta sawa na asilimia 31 ya bajeti ya maendeleo.”

Kundi lililonufaika kiasi fulani kwa bajeti hii ni wafanyakazi ambapo marekebisho katika mfumo wa kodi ya mishahara (PAYE) yamepunguzwa kiwango cha kodi hadi kufikia kima cha chini cha kodi cha asilimia 12, kutoka asilimia 13. Kundi lingine ni la wastaafu walitoa mchango mkubwa kwa Taifa hili, ambapo sasa Serikali imeona na kutambua viwango vya chini vinavyolipwa kwani haviendani na uhalisia.

“…Katika kutatua changamoto hii Serikali inapitia viwango hivyo ili kuongeza viwango kutegemeana na mapato ya Serikali na kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaendelea kuhuisha kanuni za ukokotoaji wa mafao ili kuweka ulinganifu wa mafao katika mifuko ya hifadhi ya jamii.” Alisema Waziri.