Dk Huvisa Aingia Bodi ya Chuo cha Mwalimu Nyerere, Dk Ole Medeye Apeta SADC PF

Dk. Goodluck Ole Medeye

Dk. Goodluck Ole Medeye

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemchagua Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira Dk. Terezya Huvisa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Dk Huvisa ametwaa nafasi hiyo ya kuwawakilisha wabunge katika bodi hiyo baada ya kumshinda waliyekuwa wakigombea nafasi hiyo, Mussa Haji Kombo ambaye ni mbunge wa Chama cha Wananchi, CUF.

Akitangaza matokeo hayo baada ya wabunge kupiga kura leo mjini Dodoma, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema Dk. Huvisa alipata kura 142 kati ya kura 219 zilizopigwa na wabunge huku idadi ya kura tatu akitangaza ziliharibika katika uchaguzi huo. Spika Makinda alisema katika uchaguzi huo Haji Kombo alijipatia jumla ya kura 74, hivyo kumtangaza Dk. Huvisa kushinda nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine Bunge pia lilimchagua Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Goodluck Ole Medeye kuwa mwakilishi wa Bunge la Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Madola kwa nchi za Kusini mwa Afrika, ‘SADC Parliamentary Forum’ (SADC PF).

Spika Makinda alilazimika kumtangaza Dk. Ole Medeye baada ya kuibuka na jumla ya kura 127 za wabunge na kumshinda mpinzani wake Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe aliyejipatia kura 92 kati ya jumla ya kura 222 zilizopigwa na wabunge wote huku idadi ya kura tatu zikiharibika.

Hata hivyo Dk. Ole Medeye alikuwa akitetea nafasi hiyo kwa mara nyingine kwani alikuwa ni mmoja wa wabunge wa SADC PF wanaomaliza muda wao, hivyo aliomba tena kuchaguliwa ili aendelee kuiwakilisha Tanzania na bunge lake.