TAMKO LA PAMOJA LA WABUNGE WA TANZANIA WANAOWAKILISHA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI (EALA) JUU YA SAKATA LA KUTAKA KUMVUA MADARAKA SPIKA WA BUNGE HILO 0/06/2014
Sisi, Wabunge saba wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania (EALA-TZ), tunapenda kusisitiza msimamo wetu wa kutounga mkono jaribio la kutaka kumuondoa madarakani Spika wa EALA, Mh. Margaret Nantongo Zziwa.
Baada ya kutafakari kwa uangalifu na kwa umakini mkubwa kuhusu chanzo halisi cha hoja yenyewe ya kutaka kumuondoa Spika wa EALA madarakani, tuligundua mambo yafuatavyo:
1. Hoja hii haina maslahi ya Tanzania na iko kinyume na malengo ya ushirikiano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Tumebaini kuwa hoja yenyewe ni sehemu ya “mchezo mchafu” wa ajenda ya siri ya kujaribu kuweka mbele maslahi ya baadhi ya wanachama wachache wa jumuiya badala ya kuzingatia maslahi mapana ya EAC.
2. Tuhuma mbalimbali zilizotajwa dhidi ya Spika wa EALA kuhusu yeye kuonesha upendeleaji, ujeuri na mapungufu mengine ya uongozi zimegundulika kuwa hazina mashiko na wala mantiki .
3. Kitendo ambacho kimetushtua ni kuwa kumekuwa na majaribio kadhaa ya baadhi ya Wabunge wa EALA kutoka nje ya Tanzania na viongozi wa Sekretarieti ya EAC kutaka kulazimisha sahihi za baadhi ya Wabunge wa Tanzania zitumike kinyume na utaratibu kuunga mkongo Azimio tajwa (kitu ambacho tunakipinga kwa nguvu zote). Hii inadhihirisha kuwepo kwa ajenda ya siri katika sakata hilo dhidi ya maslahi ya Tanzania na jumuiya kwa ujumla.
4. Kufuatia malumbano yaliyoibuka katika kikao cha Bunge cha mwezi Machi huko Arusha, sisi Wabunge wa Tanzania tulipokea maoni na masikitiko mengi kutoka kwa wana Afrika Mashariki na viongozi kwa ujumla wakitusihi kumaliza tatizo hili kwa njia ya amani na utulivu, lakini jitihada zetu ziligonga ukuta. Hatua hii ilizidi kutudhihirisha kuwepo kwa ajenda ya siri.
Ikumbukwe kuwa azimio la kutaka kumuondoa Spika madarakani awali lilipangiwa kuwasilishwa katika kikao cha Bunge la EALA cha mwezi Machi 2014 huko Arusha lakini liligonga mwamba baada ya kuibuka mabishano ya kisheria, hali iliyopelekea kuahirishwa kwa kikao hicho.
Hoja hii ililetwa tena kwenye vikao vingine vya EALA, lakini baada ya kutafakari kwa makini kuhusu chanzo halisi cha mzozo huu, idadi kubwa ya Wabunge kutoka Tanzania (7 kati ya 9) waliamua kwa pamoja kuipinga hoja hii kwani imekosa mashiko na haizingatii maslahi ya Tanzania na maslahi mapana ya jumuiya kwa ujumla.
Aidha, wabunge watatu wa EALA kutoka Tanzania ambao awali waliunga mkono hoja hii waliamua baadae kuipinga kwa kutoa sahihi zao kwa hiari yao wenyewe na walimwandikia barua Katibu wa Bunge wa EALA kumueleza maamuzi yao kwa mujibu wa utaratibu mnamo tarehe 29 Mei 2014. Barua hizo za Wabunge wa Tanzania wa EALA kutoa sahihi zao kwenye hoja hiyo zilipokelewa rasmi na Katibu wa Bunge.
Wabunge hao wa EALA kutoka Tanzania walitumia haki zao za kikanuni kuondoa sahihi zao kama inavyoeleza katika kanuni ya 9 (2) ya Kanuni na Utaratibu wa Uendeshaji wa Bunge (Rules of Procedure of the Assembly) inayosema: “Azimio la kumuondoa Spika madarakani halina budi kuambatana na sahihi zisizopungua nne kutoka kila nchi mwanachama.”
Hoja yenyewe ya kumuengua Spika wa EALA ni batili kisheria kwa kuwa haikuwasilishwa Bungeni ndani ya siku 7 tangu ilipopelekwa kwa Katibu wa Bunge na pia imekosa sahihi za kuungwa mkono na wabunge wanne kutoka kila nchi mwanachama wa EAC kama kanuni zinavyotamka.
Uamuzi wa Wabunge wa EALA kutoka Tanzania kuondoa sahihi zao kwenye hoja hiyo ni lazima uheshimiwe na kila mtu kwa kuwa wanatekeleza haki yao ya kidemokrasia.
Tunaomba uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ngazi zote ikiwemo Sekretarieti ya jumuiya kuheshimu maamuzi ya Wabunge wa EALA kutoka Tanzania. Ikumbukwe kuwa hapo awali, wabunge wa 5 wa EALA kutoka Tanzania kati ya jumla ya wabunge wote 9 wa Tanzania walionesha kuunga mkono hoja hii. Baada ya kubaini kuwepo kwa “mchezo mchafu” na ajenda ya siri, Wabunge watatu wa EALA kutoka Tanzania waliondoa sahihi zao na hivyo basi kufanya idadi kubwa ya Wabunge kutoka Tanzania (7 kati ya 9) kuipinga hoja hii batili.
Wabunge wa EALA wameshapoteza muda mwingi, fedha na rasilimali nyingine mpaka sasa kwenye hoja hii isiyo na tija ya kujaribu kumng’oa madarakani Spika wa EALA. Sasa hatuna budi kuweka jitihada zetu kwenye kazi muhimu ya kutetea maslahi ya raia wapatao milioni 140 wa Afrika Mashariki.
Hatuwezi kuwahudumia raia wa Afrika Mashariki kwa kuweka mbele ajenda za siri na kujishughulisha kwenye siasa za malumbano. Wananchi wa Afrika Mashariki wanataka kuona faida halisi kutoka kwenye jumuiya yao. Tuna imani na Spika wa sasa wa Bunge la EALA kuwa ni kiongozi sahihi wa kuongoza Bunge hilo.
Tunaamini kuwa hakuna tija yoyote kwa Wabunge wa EALA kuendelea kupoteza fedha za walipa kodi wa Afrika Mashariki kwa kujadili hoja hii batili. Badala yake, Wabunge wa EALA wana kazi ngumu ya kusimamia maslahi ya wananchi wa jumuiya wanaotaka kupata elimu bora, maji safi na salama ya kunywa, uhakika wa chakula, afya bora, miundombinu ya kisasa na maendeleo ya kiuchumi — siyo siasa za ulaghai.
Tunatoa wito pia kwa Wabunge wenzetu wa EALA kutoka nchi nyingine wanachama na kwa viongozi wa Sekreterieti ya EAC kutojihusisha na ajenda zozote za siri za kujaribu kumng’oa Spika wa sasa wa EALA aliyepo madarakani kisheria. Wananchi wa Afrika Mashariki wanastahili zaidi ya hayo.
Njia pekee ya kufikia maslahi yetu ya pamoja ni kwa kutumia ushirikiano, badala ya kuendekeza malumbano na siasa za chuki na kututenganisha. Sisi Wabunge saba bado tunasisitizia AMANI NA UTULIVU kwani bila ya hivyo hakuna maendeleo na ustawi wa jamii.
Tamko hili limetolewa Dar es Salaam tarehe 9 Juni 2014 na Wabunge wafuatao:
Mhe. Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa Wabunge wa EALA wa Tanzania
Mhe. Shy-rose Bhanji, Katibu wa Wabunge wa EALA wa Tanzania
Mhe. Charles Makongoro Nyerere, Mbunge wa EALA
Mhe. Maryam Ussi, Mbunge wa EALA
Mhe. Bernard Murunya, Mbunge wa EALA
Mhe. Twaha Taslima, Mbunge wa EALA
Mhe. Angellah Kizigha, Mbunge wa EALA
________________________
Mwenyekiti, Wabunge wa EALA wa Tanzania
________________________
Katibu, Wabunge wa EALA wa Tanzania
________________________
Mwanasheria, Wabunge wa EALA wa Tanzania